FADHLA YA KUSUBIRI
Ikiwa subira ni chungu mwisho wake ni tamu. Subira ndio silaha ya Muislamu ya kupambana na mitihani ya ulimwengu. Bila ya subira Muislamu hawezi kufaulu katika kufanya ibada na mambo ya akhera. Ombeni msaada kwa kusubiri na kuswali. Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) yuko pamoja na wanaosubiri. Subira huvuta kheri. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala)katika Qur’an tukufu:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اصْبِرُوا وَصَابِرُوا وَرَابِطُوا وَاتَّقُوا اللَّهَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ} آل عمران:200}
"Enyi mlio amini! Subirini, na shindaneni kusubiri, na kuweni macho, na mcheni Mwenyezi Mungu, ili mpate kufanikiwa." [Al-Imaan:200]
Jueni waja wa Mungu kuwa subira ni ukarimu usiokwisha, na ulinzi usioshindwa, na ngome isiyovunjika, subira na nusra ni ndugu wawili na asie vaa vazi la subira basi hushindwa na nafasi na sheitwani.
Subira ni ndugu yake muumini wala hana Imani kwa asie kuwa na subira, na akiwa nayo basi Imani yake ni ndogo na mtu asiekuwa na subira ni kama anavyosema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):
وَمِنَ النَّاسِ مَن يَعْبُدُ اللَّهَ عَلَىٰ حَرْفٍ ۖ فَإِنْ أَصَابَهُ خَيْرٌ اطْمَأَنَّ بِهِ ۖ وَإِنْ أَصَابَتْهُ فِتْنَةٌ انقَلَبَ عَلَىٰ وَجْهِهِ خَسِرَ الدُّنْيَا وَالْآخِرَةَ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْخُسْرَانُ الْمُبِينُ الحج:11
"Na katika watu wapo wanao muabudu Mwenyezi Mungu kwa ukingoni. Ikimfikia kheri hutulia kwayo, na ukimfikia msukosuko hugeuza uso wake. Amekhasiri dunia na Akhera; hiyo ndiyo khasara iliyo wazi." [Al-Haaj:11]
Subira ni tabia za waumini waliokamilika, hawezi kuwa nayo mtu ila baada ya kujaaliwa na Mwenyezi Mungu. Amesema Imam Ahmad; Mwenyezi Mungu ametaja subira katika Qur’an mara tisini (90) katika sehemu tofauti.
FAIDA YA KUSUBIRI
Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) atawapa malipo yao bila ya hesabu. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):
{إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُم بِغَيْرِ حِسَابٍ} الزمر:10
"Hakika wenye subira watapewa ujira wao bila ya hisabu." [Al-Zzumar:10]
Mwenyezi Mungu yuko pamoja nao katika kuwaongoza na kuwanusuru. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala)
وَأَطِيعُوا اللَّهَ وَرَسُولَهُ وَلَا تَنَازَعُوا فَتَفْشَلُوا وَتَذْهَبَ رِيحُكُمْ ۖ وَاصْبِرُوا ۚ إِنَّ اللَّهَ مَعَ الصَّابِرِينَ} الأنفال:46 {
"Na subirini. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanao subiri." [Al-Anfaal:46]
Mwenyezi Mungu kuifanya subira ni jambo la mtu Kupata uongozi. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala)
{وَجَعَلْنَا مِنْهُمْ أَئِمَّةً يَهْدُونَ بِأَمْرِنَا لَمَّا صَبَرُوا ۖ وَكَانُوا بِآيَاتِنَا يُوقِنُونَ} السجدة:24
"Na tukawafanya miongoni mwao waongozi wanao ongoa watu kwa amri yetu, walipo subiri na wakawa na yakini na Ishara zetu." [Al-Ssajda:24]
Subira ni bora kwa aliyekuwa nayo. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala)
{وَإِنْ عَاقَبْتُمْ فَعَاقِبُوا بِمِثْلِ مَا عُوقِبْتُم بِهِ ۖ وَلَئِن صَبَرْتُمْ لَهُوَ خَيْرٌ لِّلصَّابِرِينَ} النحل:126
"Na mkilipiza basi lipizeni sawa na vile mlivyo adhibiwa. Na ikiwa mtasubiri, basi hakika hivyo ni bora zaidi kwa wanao subiri." [An-Nahl:126]
Subira na Taqwa ni kinga ya vitimbi vya maadui. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala)
إِن تَمْسَسْكُمْ حَسَنَةٌ تَسُؤْهُمْ وَإِن تُصِبْكُمْ سَيِّئَةٌ يَفْرَحُوا بِهَا ۖ وَإِن تَصْبِرُوا وَتَتَّقُوا لَا يَضُرُّكُمْ كَيْدُهُمْ شَيْئًا ۗ إِنَّ اللَّهَ بِمَا يَعْمَلُونَ مُحِيطٌ} آل عمران:120
"Ikikupateni kheri huwaudhi. Na ikikupateni shari wanafurahia. Na nyinyi mkisubiri na mkajizuilia, hila zao hazitakudhuruni kitu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kuyazunguka yote wayatendayo." [Al-Imraan:120]
Subira inaleta manufaa. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala)
{يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اصْبِرُوا وَصَابِرُوا وَرَابِطُوا وَاتَّقُوا اللَّهَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ} آل عمران:200
"Enyi mlio amini! Subirini, na shindaneni kusubiri, na kuweni macho, na mcheni Mwenyezi Mungu, ili mpate kufanikiwa." [Al-Imraan:200]
Kuwabashiria Mwenyezi Mungu wenye subira kwa kheri tatu. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala)
وَلَنَبْلُوَنَّكُم بِشَيْءٍ مِّنَ الْخَوْفِ وَالْجُوعِ وَنَقْصٍ مِّنَ الْأَمْوَالِ وَالْأَنفُسِ وَالثَّمَرَاتِ ۗ وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ أُولَٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ البقرة:155-157}
"Na wabashirie wanao subiri, Wale ambao ukiwasibu msiba husema: Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake Yeye hakika tutarejea. Hao juu yao zitakuwa baraka zitokazo kwa Mola wao Mlezi na rehema. Nao ndio wenye kuongoka." [Al-Baqara:155-157]
Subira hutia mtu peponi na humuokoa kutokana na moto. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala)
إِنِّي جَزَيْتُهُمُ الْيَوْمَ بِمَا صَبَرُوا أَنَّهُمْ هُمُ الْفَائِزُونَ} المؤمنون:111 {
"Hakika Mimi leo nimewalipa kwa vile walivyo subiri. Bila ya shaka hao ndio wenye kufuzu." [Al-Muminun:111]
UHAKIKA WA SUBIRA
Subira katika lugha ya kiarabu ina maana kuzuia, na maana inayokusudiwa ni kufunga nafsi kutokana na huzuni, kuzuia ulimi kwa kushtaki, viungo kwa kupiga makofi na kupasua mifuko. Na akasema Nun Misri: “Ni kujiepusha na makosa na kutulia pindi unapopatwa na balaa na kudhihirisha utajiri pindi unapofikwa na umaskini”.
AINA ZA MASHTAKA
Mashtaka yasiyopingana na subira, kama alivyosema Mtume Yaakub. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala)
قَالَ إِنَّمَا أَشْكُو بَثِّي وَحُزْنِي إِلَى اللَّهِ وَأَعْلَمُ مِنَ اللَّهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ} يوسف:86}
"Akasema: Hakika mimi namshitakia Mwenyezi Mungu sikitiko langu na huzuni yangu." [ Yusuf:86]
Na akasema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala)
{فَصَبْرٌ جَمِيلٌ} يوسف:83
"Subira ni njema!" [Yusuf:83
Mashtaka ya saa zote na ya kusimulia
VIGAWAYO VYA SUBIRA
1. Subira katika maamrisho ya Mwenyezi Mungu
2. Subira katika makatazo ya Mwenyezi Mungu
3. Subira kutokana na kudra zake Mwenyezi Mungu.
Na kama alivyosema Sheikh AbdulKadir Jeilani: hapana budi kwa mja kufanya jambo, na kukatazika kwa jambo na kusubiri kwa Qadar.
Mambo haya matatu Luqman amemuusia mwanawe akisema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala)
{يَا بُنَيَّ أَقِمِ الصَّلَاةَ وَأْمُرْ بِالْمَعْرُوفِ وَانْهَ عَنِ الْمُنكَرِ وَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا أَصَابَكَ ۖ إِنَّ ذَٰلِكَ مِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ} لقمان:17
"Ewe mwanangu! Shika Sala, na amrisha mema, na kataza maovu, na subiri kwa yanayo kupata. Hayo ni katika mambo ya kuazimiwa." [ Luqman:17]
Muumini hatamani matatizo na anasubiri pindi anapopatwa na balaa. Mtume(Swalla Llahu ‘alayhi wasallam)siku miongoni mwa siku alipokutana na adui akimnyemelea mpaka kupinduka jua akamsimamisha akasema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam)[Enyi watu musitamani kukutana na adui na muombe Mwenyezi Mungu afya na mukikutana nao subirini na jueni kuwa pepo iko chini ya upanga].
Na Abubakar Sidiq (R.A.) amesema “Napenda kuwa na afya nishukuru ni bora kuliko kupatwa na mitihani nisubiri, na muumin anajua lolote linalompata ni kheri. Kama alivyopokea hadithi kutoka kwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) [Ajabu ya muumin ni kuwa mambo yake yote ni kheri, akipata furaha hushukuru na akipata msiba husubiri na yote ni kheri].
Maisha yote ni mitihani. Anasema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala)
{كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ ۗ وَنَبْلُوكُم بِالشَّرِّ وَالْخَيْرِ فِتْنَةً ۖ وَإِلَيْنَا تُرْجَعُونَ} الأنبياء:35
"Na tunakujaribuni kwa mtihani wa shari na kheri. Na kwetu Sisi mtarejeshwa" [Al-Anbiyaa:35]
Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) anawaonya waja wake wakati wowote ili apate kujua alie na subira na wakweli.
Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):
أَمْ حَسِبْتُمْ أَن تَدْخُلُوا الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَعْلَمِ اللَّهُ الَّذِينَ جَاهَدُوا مِنكُمْ وَيَعْلَمَ الصَّابِرِينَ} الأنبياء:142 {
"Je! Mnadhani mtaingia Peponi na hali Mwenyezi Mungu hajawapambanua wale miongoni mwenu walio pigana Jihadi, na hajawapambanua walio subiri?" [Al-Imraan:142]
Na akasema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala)
{وَلَنَبْلُوَنَّكُمْ حَتَّىٰ نَعْلَمَ الْمُجَاهِدِينَ مِنكُمْ وَالصَّابِرِينَ وَنَبْلُوَ أَخْبَارَكُمْ} محمد:31
"Na bila ya shaka tutakujaribuni mpaka tuwadhihirishe wapignao Jihadi katika nyinyi na wanao subiri. Nasi tutazifanyia mtihani khabari zenu." [Muhammad:31]
Na akasema Mwenyezi Mungu(Subhaanahu wa Taala):
إِن يَمْسَسْكُمْ قَرْحٌ فَقَدْ مَسَّ الْقَوْمَ قَرْحٌ مِّثْلُهُ ۚ وَتِلْكَ الْأَيَّامُ نُدَاوِلُهَا بَيْنَ النَّاسِ وَلِيَعْلَمَ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَيَتَّخِذَ مِنكُمْ شُهَدَاءَ ۗ وَاللَّهُ لَا يُحِبُّ الظَّالِمِينَوَلِيُمَحِّصَ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَيَمْحَقَ الْكَافِرِينَ آل عمران:141-142
"Kama yamekupateni majaraha, basi na hao watu wengine yamewapata majaraha mfano wa haya. Na siku za namna hii tunaweletea watu kwa zamu, ili Mwenyezi Mungu awapambanue walio amini na awateuwe miongoni mwenu mashahidi. Na Mwenyezi Mungu hawapendi madhaalimu; Na pia ili Mwenyezi Mungu awasafishe walio amini na awafutilie mbali makafiri" [Al-Imraan:140-141]
Na akasema mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala)
إِنَّمَا أَمْوَالُكُمْ وَأَوْلَادُكُمْ فِتْنَةٌ ۚ وَاللَّهُ عِندَهُ أَجْرٌ عَظِيمٌ} التغابن:15 {
"Hakika mali yenu na watoto wenu ni jaribio. Na kwa Mwenyezi Mungu upo ujira mkubwa." Al-Ttaghabun:15
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.