UMUHIMU WA TAWHIDI NA FADHALA ZAKE
Tawhidi ni sababu ya kuokoka mwanadamu siku ya kiama na pia kubainisha kwamba Tawhidi ni sababu ya kuondoshewa balaa na fitna
Tawhidi ni msingi mkubwa ambao Mwenyezi Mungu amewaumba majini na watu kwa ajili yake. Kwani Mwenyezi Mungu hakuwaumba majini na watu isipokuwa kwa kumuabudu yeye. Amesema Mwenyezi mungu (Subhaanahu wa Taala):
وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ} الذريات:56}
[Sikuwaumba majini na watu isipokuwa waniabudu ] [Addhariyati : 56].
Tawhidi ni jambo kubwa. Allah Subhaanahu wa Taala Amelibainisha katika kitabu chake na pia Mtume, rehma na amani zimfikie ameliweka wazi katika hadithi zake tukufu.Tawhidi ni jambo ambalo hawezi kuokoka mtu yoyote duniani na kesho Akhera ila alikamilishe jambo hilo la kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kutomshirikisha na chochote. Amesema Mtume :
من مات وهو يعلم أن لا إله إلا الله دخل الجنة] رواه مسلم]
[Atakaye kufa na akijua ya kwamba hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu ataingia peponi]. [Imepokewa na Muslim]
UMUHIMU WA TAWHIDI
Tawhidi ni jambo bora sana, na kwa sababu hii Allah (Subhaanahu wa Taala) Ameshuhudia kwa nafsi yake vile vile Malaika wameshuhudia na pia waliopewa ilimu. Na hii ni kuonesha ubora wa jambo hili la Tawhidi. Jambo Amelishuhudilia Mwenyezi Mungu(Subhaanahu wa Taala), wakashuhudia Malaika watukufu na pia wanadamu watukufu na watu waliopewa ilimu.Amesam Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Ta'aala
شَهِدَ اللَّهُ أَنَّهُ لَا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ وَالْمَلَائِكَةُ وَأُولُو الْعِلْمِ قَائِمًا بِالْقِسْطِ ۚ لَا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ} آل عمران:18}
[Ameshuhudia Mwenyezi Mungu ya kwamba hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa yeye na Malaika na pia waliopewa ilimu,hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa yeye Mwenye nguvu Mwenye hekima.] [Al-Imran : 18 ].
Miongoni mwa umuhimu wa Tawhidi ni kwamba Mtume ﷺ Alilingania Tawhidi kuanzia mwanzo wa ulinganizi wake hadi mwisho wa uhai wake, bali Mitume wote walilingania hivyo.
Pia tunapata katika sira ya Mtume ﷺ ya kwamba alipokuwa akituma maswahaba kwenda kulingania katika sehemu fulani huwausia kwanza kuwalingania watu katika Tawhidi. Yaani (Kumpwekesha Mwenzi mungu s.a)
Miongoni mwa umuhimu wa Tawhidi ni kwamba mwenye kushikamana na Tawhidi husamehewa dhambi zake na anaepushwa kukaa motoni.
Mwenye kushikamana na Tawhidi huwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu na pia hupata amani kamili na uongofu hapa duniani na kesho akhera.Mwenyezi Mungu Amesema (Subhaanau wa Ta'aala)
الَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يَلْبِسُوا إِيمَانَهُم بِظُلْمٍ أُولَٰئِكَ لَهُمُ الْأَمْنُ وَهُم مُّهْتَدُونَ} الأنعام:82}
[Wale ambao wameamini, na hawakuchanganya imani yao na dhulma - hao ndio watakao pata amani na wao ndio walio ongoka.] [Al-Anaam : 82].
Kwa mujibu wa Aya hii ni kwamba Muislamu anayeshikamana na Tawhidi atakuwa na amani hababaiki hapa duniani yuwajua litakalompata hapa duniani ni kadari ya Mola (Subhaanahu wa Taala) na kuwa atapata amani kesho akhera.
Bila ya kusahau kuwa endapo waumini watashikamana na tauhudi wataondoshewa balaa na fitna kesho akhera. Amesema Mtume ﷺ:
من شهد أن لا إله إلا الله وأن محمداً عبده ورسوله، وأن عيسى عبد الله ورسوله، وكلمته ألقاها إلى مريم وروح منه، والجنة حق، والنار حق؛ أدخله الله الجنة على ما كان من العمل رواه البخاري ومسلم
[Anayeshuhudia ya kwamba hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa yeye asiyekuwa na mshirika na Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na kwamba Nabii Isa ni mja wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na neno lake alilolitia kwa Mariam na roho kutoka kwake na pepo ni haki na moto ni haki Mwenyezi Mungu atamwingiza peponi kulingana na amali]. [Imepokewa na Bukhari na Muslim]
Ni vyema niwatajie mifano ya ambao waliepushiwa balaa na fitna.Tutoe mfano katika Mitume walioepushiwa balaa na fitna ni Nabii Ibrahiim pale walipokuwa watu wake wanataka kumchoma Mwenyezi Mungu Alimwokoa kwa kuuambia moto: “Ewe moto kuwa baridi na salama kwa Ibrahim” na ikawa kama alivyotaka Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala). Na Mtume mwengine ni Nabii Lut pale Mwenyezi Mungu Alipowaangamiza watu wake na kumwokoa yeye na waliomwamini yeye, na mifano ya walioepushiwa balaa na fitna ni mingi sana.
AINA YA TAWHIDI
Tawhidi inagawanyika sehemu tatu :
1. Tawhidu-Arrububiyah.
Tawhidi ya vitendo vya Mwenyezi Mungu s.a. nayo ni kumpwekesha Mwenyezi mungu katika uumbaji na uendeshaji wa mambo ya viumbe, na hashirikiani na yoyote katika hilo yoyote.Mwenyezi mungu anasema:
اللَّهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَأَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجَ بِهِ مِنَ الثَّمَرَاتِ رِزْقًا لَّكُمْ ۖ وَسَخَّرَ لَكُمُ الْفُلْكَ لِتَجْرِيَ فِي الْبَحْرِ بِأَمْرِهِ ۖ وَسَخَّرَ لَكُمُ الْأَنْهَارَ إبراهيم:32
[Mwenyezi Mungu ndiye aliyeumba mbingu na ardhi na ameteresha kutoka mawinguni maji akatoa kwa maji hayo mazao hali yakuwa ni riziki kweni nyinyi na akawadhalilishia majahazi ili yapite katika bahari kwa amri yake, na akawadhalilishia nyinyi mito ya maji ] [Ibrahim: 32 ].
2. Tawhidul-Uluuhiya. Nayo ni:
Tawhidi ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu katika ibada. Maana ya maneno haya ni kwamba Mwenyezi Mungu Ndiye Anayefa kuabudiwa peke yake,wala haifai kushirikishwa na yoyote.Mwenyezi Mungu (Subhaanhu wa Ta'aala)
إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ} الفاتحة:5}
[Ni wewe tu tunakuabudu na kwako wewe peke yako tunataka msaada] [Al-Faatiha : 5].
3. Tawhidul-Asmaai wa Swifaat.
Tawhidi ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu katika Sifa Zake na majina yake. Maana yake ni kwamba Mwenyezi Mungu hafanani na yoyote katika Sifa Zake na majina yake .Wala hafai yoyote kujifananisha wala kumfananisha yoyote na Mwenyezi Mungu katika sifa au majina yake kwani hana mfano wa yoyote.Asema Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Ta'aala
قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ اللَّهُ الصَّمَدُ لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ} الإخلاص:1-4}
[Sema; Mwenyezi Mungu ni mmoja Mwenyezi Mungu Ndiye Anayetakwa msaada, hakuzaa wala hakuzaliwa na Hana mfano Wake yoyote"] [Al-Ikhlas 1 - 4].
Aina zote za Tawhidi ni lazima kwa Muislamu azijue na azitumie katika maisha yake na hii ni kwa faida ya Muislamu. Na endapo mtu ataenda kinyume na aina hizi za Tawhidi basi ameshajitia matatizo duniani na kesho akhera, kwani Mwenyezi Mungu hamsamehe anayekufa katika shirki bila yakutubai.
إِنَّ اللَّهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّهِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا بَعِيدًا} النساء:116}
[Hakika Mwenyezi Mungu hasamehi kushirikishwa na kitu. Lakini Yeye husamehe yasiyo kuwa hayo kwa amtakaye. Na anaye mshirikisha Mwenyezi Mungu basi huyo amepotea upotovu wa mbali]. [An-Nisaa : 116].
MAMBO YANAYO HARIBU TAWHIDI
Miongoni mwa mambo ambayo yanatakiwa ajitahadhari nayo muislamu yasije yakamtia katika matatizo hapa dunaini na kesho akhera.
1. Ushirikina kwa aina zake zote. Kwani shirki kubwa inafutilia mbali imani ya tawhidi.
Na shirki ndogo ina punguza ukamilifu wa Tawhidi.Na mfano wa shirki ni kumuomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu jambo ambalo hana uwezo nalo isipokuwa Mwenyezi Mungu.
A. Na katika shirki kubwa ambayo tunayaona leo ni kufanya tawaf katika makaburi, (kuyazunguka makaburi)
B. kwenda kwa waganga na wachawi bali kuyaamini yote wanayoyasema kwa kudai mambo yaliofichika, na uhakika ni kwamba hakuna anayejuwa yaliofichika isipokuwa Mwenyezi Mungu na hakuna anayeweza kuleta madhara kumpata mtu isipokuwa Mwenyezi Mungu na hakuna anayeweza kuzuia kheri Akitaka Mwenyezi Mungu kuleta kheri hiyo,Mwenyezi mungu anasema:
وَإِن يَمْسَسْكَ اللَّهُ بِضُرٍّ فَلَا كَاشِفَ لَهُ إِلَّا هُوَ ۖ وَإِن يَمْسَسْكَ بِخَيْرٍ فَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ} الأنعام:17}
[Na ikiwa Mwenyezi Mungu akikugusisha madhara, basi hapana wa kukuondolea hayo ila Yeye. Na ikiwa akikugusisha kheri, basi Yeye ndiye Mwenye uweza wa kila kitu.] [ Al-Anaam : 17].
Kwa hivyo, tujue ya kwamba Mwenyezi Mungu Ndiye anayeleta manufaa na madhara, na kwa sababu hiyo yatakiwa Mwenyezi Mungu aogopewe haki ya kuogopewa.
C. Na aina za shirki ni mtu kuomba dua kumuomba mtu jambo ambalo hakuna awezaye kulifanya isipokuwa Mwenyezi Mungu kama kuondoa ugonjwa. Huku tukijua ya kwamba dua ni ibada, kwa hivyo, ibada hiyo ya dua haifai kufanyiwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu.
D. Aina nyingine ya shirki kubwa ni ushirikina katika nia na makusudio, hii ni mtu kunuwia au kufanya ibada kwa kutaka au kukusudia mambo ya kidunia au wamuone kwamba yuwafanya ibada au watu wamsikie au apate sifa kwa watu,Mwenyezi Mungu anasema:
مَن كَانَ يُرِيدُ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا وَزِينَتَهَا نُوَفِّ إِلَيْهِمْ أَعْمَالَهُمْ فِيهَا وَهُمْ فِيهَا لَا يُبْخَسُونَ أُولَٰئِكَ الَّذِينَ لَيْسَ لَهُمْ فِي الْآخِرَةِ إِلَّا النَّارُ ۖ وَحَبِطَ مَا صَنَعُوا فِيهَا وَبَاطِلٌ مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ هود:15-16
[Wanao taka maisha ya dunia na pumbao lake tutawalipa humo vitendo vyao kaamili. Na wao humo hawatopunjwa. Hao ndio ambao hawatakuwa na kitu Akhera ila Moto, na yataharibika waliyo yafanya, na yatapotea bure waliyo kuwa wakiyatenda.] [Huud : 15 - 16].
Haya ni malipo ya wanaofanya ibada kwa ajili ya kuonekana na watu na kwa ajili ya dunia.
E. Aina nyingine ni shirki ya kutii viongozi wa dini kinyume na miongozo sahihi ya Uislamu katika kuhalalisha vilivyoharamishwa na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala).
اتَّخَذُوا أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّهِ} التوبة:31}
[Wamewafanya makuhani wao na wamonaki wao kuwa ni marabi badala ya Mwenyezi Mungu,] [Tawba : 31].
Mtume ﷺ Alimfasiria Adiy bin Hatiim ibada yenu kwao ni kumtii katika kumuasi Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala).kuhalalisha yalio haramiswa na Mwenzi Mungu.
KWA FAIDA ZAIDI SIKILA MADA HII NA SHEIKH SHADDAD
UCHAJI MWENYEZI MUNGU NA ATHARI ZAKE
Ni nini uchaji mungu?. Ni kujiepusha na kila ambalo Mwenyezi Mungu halitaki na kutekeleza kila jambo ambalo Mwenyezi Mungu analipenda. Vile vile, uchaji Mungu ni kujilinda na adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa kufanya vitendo vizuri, na kuogopa kwa siri na kwa dhahiri. Na kuogopa. Ni kama alivyosema Ali Bin Abi Twalib: ‘ Ni kumuogopa Mola, na kutumia Qur’an, na kuridhika na kidogo, na kujianda kwa siku ya safari’. Imekuja ya kwamba ‘Umar Bin Khatwab radhi za Mwenyezi Mungu zimfikie alimuuliza Ubayyah Bin Ka’ab: Taqwa ni nini? Akamwambia: Je umefuata njia ya miba? Akamwambia kwa nini? Hukujua? Akasema nilitembea kwa hadhari kuogopea miba kunidunga. Akasema hiyo ndiyo taqwa’.
Kumuogopa Mwenyezi Mungu ni mkusanyiko wa kheri na mambo mengi yametajwa katika Qur’an tukufu. Hakuna kheri yoyote ya dunia na akhera wala ya ndani na nje ila Taqwa imeshikanishwa nazo. Na hakuna shari yoyote ya dunia na akhera wala ya ndani na nje ila Taqwa imekuwa mbali nayo. Na katika kheri za Taqwa ni kufunguliwa milango ya kheri, na kwa Taqwa hufunzwa usioyajua.
Taqwa ni wasia wa watu wa mwanzo na wa mwisho. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala)
إِن تَجْتَنِبُوا كَبَائِرَ مَا تُنْهَوْنَ عَنْهُ نُكَفِّرْ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَنُدْخِلْكُم مُّدْخَلًا كَرِيمًا} النساء:131}
[Na kwa hakika tuliwausia waliopewa kitabu kabla yenu, na nyinyi pia, kwamba mumche Mwenyezi Mungu ] [Nisaa : 131]
Na Taqwa ni Mwito wa Mitume na alama ya waja wema. Kila Mtume alikuwa akiwaambia watu wake:
أَلَا تَتَّقُونَ} الشعراء:124}
[Je hamumuogopi Mungu] [Ashuaraa :124]
Taqwa asli yake ni kinga baina ya mja na lile analoliogopa na kujitahadhari nalo. Na Mola wetu mtukufu ndiye Anaye stahiki kuogopewa nayeye pekee ndiye Anayetukuzwa. Kama Alivyosema Ali Radhi za Mwenyezi Mungu juu yake ‹Taqwa ni kumuogopa Mwenyezi Mungu na kutumia kitabuchake (Qur’an) na kutosheka na kichache na kujiandalia siku ya safari›.
SIFA ZA WACHAJI MUNGU.
Sifa za wanaomuogopa Mwenyezi Mungu. Katika sifa za wanaomuogopa Mungu (Subhaanahu wa Taala):
1. Kuamini mambo ya siri (ghaib)
2. Kusimamisha Swala kwa wakati wake.
3. Kutoa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.
4. Kuamini Aliyoteremsha Mwenyezi Mungu(Subhaanahu wa Taala).
5. Kuwa na yakini na Siku ya Akhera. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala)
الم ذَٰلِكَ الْكِتَابُ لَا رَيْبَ ۛ فِيهِ ۛ هُدًى لِّلْمُتَّقِينَ الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِالْغَيْبِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ وَالَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ وَمَا أُنزِلَ مِن قَبْلِكَ وَبِالْآخِرَةِ هُمْ يُوقِنُونَ أُولَٰئِكَ عَلَىٰ هُدًى مِّن رَّبِّهِمْ ۖ وَأُولَٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ
[Alif laam miim Hiki ni kitabu hakina shaka ndani yake ni ongofu kwa wanaomcha Mwenyezi Mungu. Ambao huyaamini yasioonekana na husimamisha swala na hutoa zile tulizowapa. Na ambao wanaamini yaliyo teremshwa kwako na yaliyoteremshwa kabla yako na wanaamini Akhera. Hao wako juu ya ongofu utokao kwa Mola wao na hao ndio waongufu"] [Al-Baqara : 1 - 5]
6. Kutekeleza ahadi na kusubiri wakati wa raha au shida. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala)
لَّيْسَ الْبِرَّ أَن تُوَلُّوا وُجُوهَكُمْ قِبَلَ الْمَشْرِقِ وَالْمَغْرِبِ وَلَٰكِنَّ الْبِرَّ مَنْ آمَنَ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَالْمَلَائِكَةِ وَالْكِتَابِ وَالنَّبِيِّينَ وَآتَى الْمَالَ عَلَىٰ حُبِّهِ ذَوِي الْقُرْبَىٰ وَالْيَتَامَىٰ وَالْمَسَاكِينَ وَابْنَ السَّبِيلِ وَالسَّائِلِينَ وَفِي الرِّقَابِ وَأَقَامَ الصَّلَاةَ وَآتَى الزَّكَاةَ وَالْمُوفُونَ بِعَهْدِهِمْ إِذَا عَاهَدُوا ۖ وَالصَّابِرِينَ فِي الْبَأْسَاءِ وَالضَّرَّاءِ وَحِينَ الْبَأْسِ ۗ أُولَٰئِكَ الَّذِينَ صَدَقُوا ۖ وَأُولَٰئِكَ هُمُ الْمُتَّقُونَ
[Bali wema ni wale wanaomuamini Mwenyezi Mungu na siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Mitume na wanawapa mali – juu ya kuwa wanayapenda- jamaa na mayatima na maskini na wasafiri na waombao na kuwakomboa watumwa na wanasimamisha swala na kutoa zaka, na watekelezao ahadi zao wanapoahidi, na wavumiliao katika shida na raha na wakati wa vita ] [AL-Baqarah : 177]
7. Kuomba msamaha kwa madhambi yao. Kama Alivyosema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):
وَالَّذِينَ إِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً أَوْ ظَلَمُوا أَنفُسَهُمْ ذَكَرُوا اللَّهَ فَاسْتَغْفَرُوا لِذُنُوبِهِمْ وَمَن يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلَّا اللَّهُ وَلَمْ يُصِرُّوا عَلَىٰ مَا فَعَلُوا وَهُمْ يَعْلَمُونَ آل عمران:135
[Na wale ambao wanapofanya uchafu au kudhulumu nafsi zao hukumbuka Mwenyezi Mungu na kuomba msamaha kwa dhambi zao ] [Al-Imraan : 135].
FADHILA ZA TAQWA
Taqwa hufungua moyo. Kama Alivyosema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):
{وَاتَّقُوا اللَّهَ ۖ وَيُعَلِّمُكُمُ اللَّهُ} {البقرة:282}
[Muogopeni Mwenyezi Mungu atawafundisha nyinyi"] [Al-Baqarah : 282]
Amesema Mola(Subhaanahu wa Taala):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تَتَّقُوا اللَّهَ يَجْعَل لَّكُمْ فُرْقَانًا وَيُكَفِّرْ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ۗ وَاللَّهُ ذُو الْفَضْلِ الْعَظِيمِ} الأنفال:29}
[Enyi mlioamini mkimuogopa Mwenyezi Mungu atawapa ufafanuzi kufafanua baina ya haki na batili na atakufutieni makosa yenu,na kukusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kubwa kabisa] [Anfal : 29]
Kupata kabuli. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):
وَيُنَجِّي اللَّهُ الَّذِينَ اتَّقَوْا بِمَفَازَتِهِمْ لَا يَمَسُّهُمُ السُّوءُ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ} الزمر:61}
[Na Mwenyezi Mungu Atawaokowa wale wamchao kwa ajili ya kufaulu kwao hawataguswa na ubaya na wala hatahuzunika ] [Azumar : 61]
Kuokoka na moto na kufaulu kwa nyumba ya furaha. Amesema Allah (Subhaanahu wa Taala):
تِلْكَ الْجَنَّةُ الَّتِي نُورِثُ مِنْ عِبَادِنَا مَن كَانَ تَقِيًّا} مريم:63}
[Hiyo nidiyo pepo tutakayowarithisha katika waja Wetu wale ambao ni wachaji Mungu] [Maryam : 63]
Mwenyezi Mungu Atujaalie katika wale wanao muogopa Mwenyezi Mungu nakupata msamaha wake Allah. Muombeni msamaha Yeye peke yake. Hakika Yeye ndie Mwenye kusamehe waja wake wote.
SIKILIZA MADA HII NA SHEIKH HASSAN SUGO
NEEMA YA PEPO NA ADHABU YA MOTO
Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Ambaye Ameumba pepo na moto. Mwenye kufanya wema ataingizwa peponi, na Mwenye kufanya mabaya ataingizwa motoni.
Ni nini neema? kila linalo takiwa na kupendeza huitwa neema. Lakini neema ya uhakika ni kufaulu Akhera na kuingia peponi. Pepo ni nyumba ilyo andaliwa watu wema ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala), ndani kuna majumba na mashamba yaliyo na miti tofauti, na mito aina mbali mbali.
Ndugu muislamu katika makala haya mafupi tutaelezea juu ya bidhaa iliyo ghali haipati bidhaa hiyo ila aliye rehemewa na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala). Wanaikimbilia biashara hiyo kila mmoja wetu sawa akiwa mume au mke, ni bidhaa iliyo na thamani kubwa inatafutwa na kila mtu. walienda mbio waliopita katika Waislamu na mpaka Waislamu wa sasa kwa lengo la kupata bidhaa hiyo. Na bidhaa hiyo si nyingine bali ni PEPO, iliyo andaliwa wale wote wenye vitendo vyema. Kama pepo ilivyo andaliwa kwa watu wema, vile vile Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala)akauandaa moto kwa makafiri na wanafiki na kila anayemuasi Mwenyezi Mungu. Na pepo ni ya wanaomcha Mwenyezi Mungu, na moto ni ya wanaomuasi Mwenyezi Mungu. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):
وَسَارِعُوا إِلَىٰ مَغْفِرَةٍ مِّن رَّبِّكُمْ وَجَنَّةٍ عَرْضُهَا السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ أُعِدَّتْ لِلْمُتَّقِينَ} آل عمران:133}
[Na yakimbilieni maghfira ya Mola wenu Mlezi, na Pepo ambayo upana wake ni mbingu na ardhi, iliyo wekwa tayari kwa wachamngu] [Al-Imran:133].
Na Akasema tena Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala)
فَإِن لَّمْ تَفْعَلُوا وَلَن تَفْعَلُوا فَاتَّقُوا النَّارَ الَّتِي وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ ۖ أُعِدَّتْ لِلْكَافِرِينَ } البقرة:24}
[Na mkitofanya - na wala hamtofanya kamwe basi uogopeni moto ambao kuni zake ni watu na mawe walio andaliwa hao wanao kanusha] [Al-Baqarah : 24]
Hakika pepo ni nyumba ya wachaji Mungu. Nyumba iliyo neemeshwa imeandaliwa watu wema miongoni mwa Mitume na wa kweli na mashahidi pepo inayo pita chini yake mito, na nyumba ambazo kuta zake ni dhahabu na fedha, ndani yake mna wake wema walio wazuri, ndani yake watu wanakula wala hawaendi haja, kunao ndani ya pepo walio neemeshwa wana furaha siku zote wala hawapati huzuni wanacheka na wala hawalii watakuwa hai siku zote na wala hawatokufa. Nyuso zao zina furaha, ndani yake mna Hurul-‘Ain. Bali watu wa peponi wana neema zaidi na zaidi kwenye pepo mna mambo jicho halijaona wala sikio halijasikia. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):
فَلَا تَعْلَمُ نَفْسٌ مَّا أُخْفِيَ لَهُم مِّن قُرَّةِ أَعْيُنٍ جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ} السجدة:17}
[Nafsi yoyote haijui waliyo fichiwa katika hayo yanayo furahisha macho - ni malipo ya yale waliyo kuwa wakiyatenda.] [Assajdah : 17]
NEEMA ZA PEPO KATIKA HADITHI ZA MTUME ﷺ
Na Hadithi nyingi za Mtume ﷺ zimebainisha hayo. Imepokewa na Abi Hurayra, Akipokea kutoka kwa Mtume ﷺ Anasema: Mwenyezi Mungu alie mshindi na mwenye nguvu:
أَعْدَدْتُ لِعِبَادِي الصَّالِحِينَ مَا لَا عَيْنٌ رَأَتْ وَلَا أُذُنٌ سَمِعَتْ وَلَا خَطَرَ عَلَى قَلْبِ بَشَرٍ ذُخْرًا بَلْهَ مَا أُطْلِعْتُمْ عَلَيْهِ] رواه البخاري ومسلم]
[Nime waandalia waja wangu wema neema ambao jicho halijaona na wala sikio halijasikia na wala haipiti fikra katika moyo wa mwanadamu] [Imepokelewa na Bukhari na Muslim]
Vile vile imekuja katika Hadithi za Mtume ﷺ Ameipokea Abu Hurayra Amesema Mtume ﷺ:
أول زمرة يدخلون الجنة على صورة القمر ليلة البدر ، والذين يلونهم على صورة أشد كوكب دري في السماء إضاءة ، لا يبولون ، ولا يتغوطون ، ولا يتفلون ولا يمتخطون ، أمشاطهم الذهب ، ورشحهم المسك ، ومجامرهم الألوة ، وأزواجهم الحور العين ، أخلاقهم على خلق رجل واحد ، على صورة أبيهم آدم ، ستون ذراعا في السماء رواه البخاري ومسلم
[Hakika [Kundi la kwanza Litakaloingia peponi litaingia kama mwezi wa kumi na nne na wanaofuatia ni kama nyota iliyo mbinguni kwa muangaza wake hawakojoi wala hawaendi haja kubwa wala hawatemi mate wala makohozi vichana vyao ni vya dhahabu pafumu yao ni miski wake zao ni Hurul-‘Ain umbile lao ni moja kwa sura ya baba yao Adam dhiraa sitini kwenda juu.] [Imepokewa na Bukhari na Muslim]
Amesema Mtume ﷺ:
[Anayeingia peponi atastarehe wala hangonjeki, wala nguo yake hairaruki wala hawi mzee] [Muslim]
Vilevile katika kuonesha neema za peponi ni Hadithi ya Abu-Said Al-Khudhriyi na Abu Hurayrah wakipokea kwa Mume ﷺ Amesema:
يُنَادِي مُنَادٍ -يعني في أهل الجنة- : إِنَّ لَكُمْ أَنْ تَصِحُّوا فَلا تَسْقَمُوا أَبَدًا ، وَإِنَّ لَكُمْ أَنْ تَحْيَوْا فَلا تَمُوتُوا أَبَدًا ، وَإِنَّ لَكُمْ أَنْ تَشِبُّوا فَلا تَهْرَمُوا أَبَدًا ، وَإِنَّ لَكُمْ أَنْ تَنْعَمُوا فَلا تَبْأَسُوا أَبَدًا رواه مسلم
[Atalingania mwenye kulingania Aseme: Hakika uzima ni wenu na hamtakuwa wagonjwa kabisa, na hakika ni wenu nyinyi uhai hamtokufa kabisa, na hakika ni wenu nyinyi ubarobaro hamtakuwa wazee kabisa, na hakika ni zenu nyinyi starehe hamtakuwa na shida kabisa.] [Imepokewa na Muslim]
[Na wataitwa waambiwe hiyo ndiyo pepo mlio ridhishwa ni malipo yale mliyoyafanya].
MOTO NA WATU WAMOTONI
Baada ya kuzungumzia watu wa peponi na starehe zao. Kidogo tuizungumzie hali ya watu wa motoni na sifa zao na hali ya moto, ndani ya moto mna vinywaji vikali. Hakika moto ni nyumba ya watu wabaya, na ni nyumba ya adhabu kama Alivyosema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):
لَهُمْ شَرَابٌ مِّنْ حَمِيمٍ وَعَذَابٌ أَلِيمٌ بِمَا كَانُوا يَكْفُرُونَ} الأنعام:70}
[Wao watapata kinywaji cha maji ya moto kabisa, na adhabu chungu ] [An-Aam : 70].
Na Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):
وَالَّذِينَ كَفَرُوا لَهُمْ شَرَابٌ مِّنْ حَمِيمٍ وَعَذَابٌ أَلِيمٌ بِمَا كَانُوا يَكْفُرُونَ} يونس:4}
[Na walio kufuru, wao watapata vinywaji vinavyo chemka, na adhabu chungu kwa sababu ya walivyo kuwa wakikufuru.] [Yuunus : 4]
Kwa hivyo, Moto ni mahali pa watu wabaya wanaokosea amri ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala). Kama Alivyosema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):
هَٰذَا ۚ وَإِنَّ لِلطَّاغِينَ لَشَرَّ مَآبٍ جَهَنَّمَ يَصْلَوْنَهَا فَبِئْسَ الْمِهَادُ} ص:55-56}
[Ndio hivi! Na hakika wenye kuasi bila ya shaka watapata marudio maovu kabisa, Nayo ni Jahannamu! Wataingia humo. Nacho hicho ni kitanda kiovu mno cha kulalia] [Saad : 55-56].
Na katika kukamilisha kuelezea habari ya moto na sifa zake ni Hadithi ya Shaqiq. Imetokana na shaqiq amepokea kwa ‘Abdillahi Akisema: Amesema Mtume ﷺ
يؤتى بجهنم يوم القيامة لها سبعون ألف زمام مع كل زمام سبعون ألف ملك يجرونها] رواه مسلم]
[Utaletwa moto siku hiyo umefungwa vifungo sabini elfu na kila kifungo kimoja kina vutwa na Malaika sabini elfu, wanauburuza] [Imepokewa na Muslim]
Tunamuomba Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Atuepushe na moto wa Jahannam Atujaalie ni katika wenye kusikia mema pamoja na kuyafuata.
SIKILIZA MADA HII NA SHEIKH HASSAN SUGO
KUMPENDA MWENYEZI MUNGU (SUBHAANAHU WA TA'AALA)
Ni nini mapenzi? Mapenzi ni jambo ambalo watu wana shindana katika kupenda kitu. Mapenzi huonyesha ukweli wa mwenye kupenda kitu. Na tukisema kumpenda Mwenyezi Mungu na Mtume ni vipi? Ni kufuata kila walilo amrisha na kuacha kila walilo kataza, kama ilivyo kuja katika Qur’an.Mwenyezi Mungu (Subhanahu wa T'aala) Aseama:
وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ۚ وَاتَّقُوا اللَّهَ ۖ إِنَّ اللَّهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ} الحشر:7}
[Na anacho kupeni Mtume chukueni, na anacho kukatazeni jiepusheni nacho. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu] [ Al-Hashri:7]
Ndugu Muislamu, mada kama hii ni muhimu kwa kila Muislamu na inahitajia kila mmoja wetu, bali kuhakikisha yanayolazimu imani, hakuna imani kwa yeyote ambae hatahakikisha hilo, nalo si lingine ni Mapenzi ya Mwenyezi Mungu na Mtume wetu ﷺ na kuwaweka mbele kuliko yoyote.
Hakika mapenzi ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake ni katika imani. Hawi muumini yoyote ila atangulize mapenzi ya kumpenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake kuliko chochote alichokimiliki mali, watoto, wazazi na watu wote. Kama alivyo toa khabari juu ya hilo Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):
قُلْ إِن كَانَ آبَاؤُكُمْ وَأَبْنَاؤُكُمْ وَإِخْوَانُكُمْ وَأَزْوَاجُكُمْ وَعَشِيرَتُكُمْ وَأَمْوَالٌ اقْتَرَفْتُمُوهَا وَتِجَارَةٌ تَخْشَوْنَ كَسَادَهَا وَمَسَاكِنُ تَرْضَوْنَهَا أَحَبَّ إِلَيْكُم مِّنَ اللَّهِ وَرَسُولِهِ وَجِهَادٍ فِي سَبِيلِهِ فَتَرَبَّصُوا حَتَّىٰ يَأْتِيَ اللَّهُ بِأَمْرِهِ ۗ وَاللَّهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْفَاسِقِينَ
[Sema: Ikiwa baba zenu, na wenenu, na ndugu zenu, na wake zenu, na jamaa zenu, na mali mliyo yachuma, na biashara mnazo ogopa kuharibika, na majumba mnayo yapenda, ni vipenzi zaidi kwenu kuliko Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Jihadi katika Njia yake, basi ngojeni mpaka Mwenyezi Mungu alete amri yake. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wapotovu.] [ Tawab : 24]
Amesema Qaadhi ‘Iyadh Mungu Amuwee radhi Inatosha Aya hii kuwa ni tanabahisho na ni dalili kubwa na ni huja juu ya ulazima wa mapenzi ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake.
Na kuonyesha uwajibu wake na ni haki kumpenda Mtume ﷺ. Wakati Mwenyezi Mungu Alipotangaza yoyote atakaye kuwa mali yake, watoto wake, mke wake ni bora kuliko Mwenyezi Mungu na Mtume, kisha akawaahidi adhabu kali, kwa kusema: "Ngojeni amri ya Mwenyezi Mungu ije.
Kisha Akakamilisha Aya kwa kuwaita maasi, na Mwenyezi Mungu hawaongozi mafasiki.
Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):
قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَاللَّهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ} آل عمران:31}
[Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu basi nifuateni mimi, Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakufutieni madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta madhambi na Mwenye kurehemu.] [Al-Imran : 31]
Amesema tena Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُقَدِّمُوا بَيْنَ يَدَيِ اللَّهِ وَرَسُولِهِ ۖ وَاتَّقُوا اللَّهَ ۚ إِنَّ اللَّهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ} الحجرات:1}
[Enyi mlio amini! Msitangulie mbele ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.] [Al-Hujrat : 1]
Na kama ilivyo kuja katika Hadith. Imepokelewa na Anas (R.A.) Akisema: Amesema Mtume ﷺ:
لا يؤمن أحدكم حتى أكون أحبَّ إليه من ولده ووالده والناس أجمعين] رواه البخاري ومسلم]
[Hawi na imani mmoja wenu mpaka anipende zaidi mimi kuliko mzazi wake na mtoto wake na watu wote] [Imepokewa na Bukhari na Muslim]
Amepokea Anas kutoka kwa Mtume ﷺ akisema:
ثلاثٌ من كن فيه وجد بهن حلاوة الإيمان، من كان الله ورسوله أحبَّ إليه مما سواهما، وأن يحب المرء لا يحبه إلا لله، وأن يكره أن يعود في الكفر بعد أن أنقذه الله منه، كما يكره أن يقذف في النار رواه البخاري ومسلم
[Mambo matatu ukiwa nayo unapata utamu wa imani; Ni kumpenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake zaidi kuliko wengine. Na asimpende mtu ila kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Na achukie kurudi katika ukafiri kama anavyo chukia kuingia motoni] [Imepokewa na Bukhari na Muslim]
Na mapenzi ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake yanao alama za kujulisha mapenzi yao. Wamezitaja na wakazibainisha Wanachuoni, zimetolewa katika Qur›an na sunnah na miongoni wa alama hizo:
ALAMA ZA KUJULISHA MAPENZI KWA MTUME ﷺ
1. Ni kufuata Kitabu cha Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala).
2. Ni kutekeleza Sunnah zake zote, kwa kumfuata Mtume na kufanya sunnah zake na kufuata maneno yake na vitendo vyake.
3. Na kufuata maamrisho yake na kujiepusha na makatazo yake na kujipamba kwa adabu za Mtume katika uzito na wapesi. Amesema Qaadhi Iyadh:R.A ‘Mwenye kupenda jambo huathirika na huathirika kwa kuliafiki. Asipokuwa hivyo, huwa si mkweli katika mapenzi yake.
Kuathirika na aliyoweka Mwenyezi Mungu na kujiepusha na mapenzi ya nafsi na kufuata matamanio.
KWA FAIDA ZAIDI SIKILIZA MADA HII NA SHEIKH YUSUF ABDI
KUTAHADHARI NA UCHAWI NA UGANGA
Ndugu Muislamu katika Makala haya tutaelezea hukumu ya uchawi na uganga katika uislamu pia tutatoa tahadhari kwa watu kwenda kwa waganga na wapiga ramli na pia tuwabainishie hatari za waganga katika umma tutahimiza kuchukua sababu za kisheria.
Ni kweli usiofichika ya kwamba watu wanapitia mitihani mbali mbali, kwa mfano mitihani ya kiuchumi, ya kiafya na pia ya kijamii na mitihani mingineo. Kwa hivyo kukabiliana na mitihani hii ni lazima sheria ichungwe na sababu za kisheria zifuatwe katika kutatua matatizo yoyote yanayomkabili Muislamu popote alipo hafai kwenda kinyume na sheria.
Ndugu Muislamu hakika katika mitihani waliopewa watu leo, waume kwa wake, wakubwa kwa wadogo, isipokuwa walio rehemewa na Mwenyezi Mungu ni kwenda kwa waganga na watu wa ramli wanaokula mali ya watu kwa batili.
Unaweza kumuona kiongozi amefungamanishwa na mganga hafanyi jambo lolote isipokuwa kwa ushauri wake hata kama ushauri huo utaenda kinyume na dini ya kiislamu, na anahisi ndani ya moyo wake ya kwamba huyo mganga ndiye anayempa uongozi na anaweza kuuchukua uongozi huo.na Kusahau kabisa kuwa Mwenyezi Mungu (Subhanahu wa Ta'aala) Ndie mmiliki wa kila kitu,Mwenyezi Mungu Anasema:
قُلِ اللَّهُمَّ مَالِكَ الْمُلْكِ تُؤْتِي الْمُلْكَ مَن تَشَاءُ وَتَنزِعُ الْمُلْكَ مِمَّن تَشَاءُ وَتُعِزُّ مَن تَشَاءُ وَتُذِلُّ مَن تَشَاءُ ۖ بِيَدِكَ الْخَيْرُ ۖ إِنَّكَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ آل عمران:26
[Sema ewe Mwenyezi Mungu Mfalme wa wafalme Unampa ufalme unaye mtaka na unampokonya ufalme unayemtaka na unamtukuza unayemtaka na Unamdhalilisha unayemtaka katika mkono wako kuna kheri. Hakika yako wewe juu ya kila kitu ni muweza] [Al-Imraan: 26]
Utaona mfanyabiashara hanunui wala hauzi isipokuwa kwa ushauri wa mganga ambaye amefungamanisha moyo wake na mganga huyo na hufanya lolote atakaloambiwa na mganga namna litakavyokuwa jambo lile.
Utapata mke anaetaka kumtawala mumewe kwa kiasi ambacho mume yule hatatamani mke mwengine isipokuwa yeye ataenda mke yule kwa mganga mchafu na atataka usaidizi, akisahau kuwa Mwenyezi Mungu ndie ambaye amejaalia mapenzi ya dhati baina ya mume na mke hii ndio hali yetu waja wa Mwenyezi Mungu isipokuwa aliyerehemewa na Mwenyezi Mungu.
Ndugu katika imani ni vyema kila Muislamu kujuwa Hukmu ya kufanya hivyo,na kwamba Mwenyezi Mungu Amebainisha wazi katika Qur’an tukufu kwamba kujifundisha uchawi ni ukafiri.
Mwenyezi Mungu (Subhanahu wa Ta'aala)
وَمَا يُعَلِّمَانِ مِنْ أَحَدٍ حَتَّىٰ يَقُولَا إِنَّمَا نَحْنُ فِتْنَةٌ فَلَا تَكْفُرْ} البقرة:102}
[Na hawamfundishi yoyote mpaka waseme hakika yetu sisi ni fitna usikufuru ] [Al-Baqara: 102]
Na vile vile Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Amesema:
وَلَا يُفْلِحُ السَّاحِرُ حَيْثُ أَتَىٰ} طه:69}
[Na mchawi hafanikiwi popote afikapo.] [Twaha: 69].
Na amesema Mtume ﷺ:
اجتنبوا السبع الموبقات))، قالوا: يا رسول الله، وما هن؟ قال: ((الشرك بالله، والسحر، وقتل النفس التي حرم الله إلا بالحق، وأكل الربا، وأكل مال اليتيم، والتولي يوم الزحف، وقذف المحصنات المؤمنات الغافلات متفق عليه
[Jiupusheni na mambo saba yanayoangamiza, wakasema maswahaba: Ni yapi, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Akasema Mtume ﷺ: Kumshirikisha Mwenyezi Mungu, na uchawi, na kuuwa nafsi aliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu ila kwa haki, na kula Ribaa, na kula mali ya yatima, na kukimbia vitani,(katika jihadi) na kuwasingizia kuwa wamezini wanawake waliojihifadhi walioghafilika tena waumini]. [Imepokewa na Bukhari na Muslim]
Asema Aisha:Watu walimuuliza Mtume ﷺ kuhusu uganga akasema: [Hao si chochote. Wakasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu hakika hao wanazungumzia mambo mara nyingine kisha yanatokea kweli. Akasema Mtume ﷺ:
تِلْكَ الْكَلِمَةُ الْحَقُّ يَخْطَفُهَا الْجِنِّيُّ ، فَيَقْذِفُهَا فِي أُذُنِ وَلِيِّهِ ، وَيَزِيدُ فِيهَا مِائَةَ كَذْبَةٍ] رواه مسلم]
[Hilo ni neno la haki analolichukua jinni kisha akalitia katika sikio la rafiki yake naye kwa upande wake akachanganya neno hilo na maneno mia ya uongo]. [Imepokewa na Muslim]
Na katika hadithi nyingine za kukataza uchawi na uganga. Mtume
ﷺ: amesema:
مَنْ أَتَى كَاهِنًا، أَوْ عَرَّافًا، فَصَدَّقَهُ بِمَا يَقُولُ، فَقَدْ كَفَرَ بِمَا أُنْزِلَ عَلَى مُحَمَّدٍ صلى الله عليه وسلم] رواه أحمد]
[Atakayeenda kwa mganga au mchawi akamuuliza na akamuamini kwa atakayosema basi amekufuru aliyoteremshiwa Mtume Muhammad rehma na amani zimfikie]. [Imepokewa na Ahmad]
Hadithi hii tukufu inatufundisha kwamba mtu yoyote atakaye kwenda kwa mganga kumuuliza kitu na akamuamini kwa atakayomwambia basi ametoka kabisa katika dini ya Uislamu. Ama hukumu ambayo inatakiwa aichukue kiongozi kwa atakayepatikana anafanya uchawi ni kukatwa shingo yake na kuuwawa kama ilivyothibiti katika maneno ya Maswahaba Mwenyezi Mungu awawie radhi; Tahadhari tunayoitoa ni kwamba haifai kwa Muislamu kuchukua hatua mikononi mwake isije ikaleta balaa na fujo miongoni mwa watu.
MADHARA YA WACHAWI NA WAGANGA KATIKA UMMA
Baadhi ya madhara ya waganga na wachawi katika umma. Madhara hayo ni kama yafuatayo;
1. Kufutika imani za wanaokwenda kwa waganga na kuwaamini kwa watakayo ambiwa kama ilivyo katika hadithi ya Mtume ﷺ tuliyoitaja.
2. Kukithiri vifo na au kuona makaburi yanafukuliwa au kuona baadhi ya viungo vya wanadamu kwa hawa waganga baada ya kuwaamrisha wafuasi wao wawaletee.
3. Kuenea zina na machafu baina ya watu kwani ni wangapi katika waganga hufanya zina na wake za watu na wakaharibu ndoa za watu na wakafungua milango mikubwa ya shari.
4. Kula mali za watu kwa njia ya batili kinyume na haki, kwani kila anachochukua mganga ni kwa kazi yake mbovu na anakula uchafu. Mtume ﷺ amekataza kula thamani ya mbwa na mahari ya mzinifu na chumo la mganga.
5. Kuwapoteza watu na kuwafanya watu kuwa na tabia mbaya na kuwazuia wao kutekeleza maamrisho ya Dini, kwani kuna wengine huacha swala zote au baadhi yake na wengine huzuiliwa kuoga janaba na wengine huzuiliwa kufanya mema bali huamrishwa kufanya mabaya.
6. Kumkasirisha Mwenyezi Mungu na kusababisha adhabu yake. Alisema Zainab binti Jahshi kumwambia Mtume ﷺ:
أَنَهْلِكُ وَفِينَا الصَّالِحُونَ قَالَ « نَعَمْ إِذَا كَثُرَ الْخَبَثُ] رواه مسلم]
[Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Je tunaweza kuangamizwa na kati yetu kuna watu wema? Akasema Mtume ﷺ: Ndio, ukikithiri uchafu]. [Imepokewa na Muslim]
Na je kuna wachafu zaidi kuliko waganga waovu?.
7. Kupata hasara duniani na kesho akhera.Amesema Mwenyezi Mungu (Subhanahu wa Ta'aala)
وَلَا يُفْلِحُ السَّاحِرُ حَيْثُ أَتَىٰ} طه:69}
[Na mchawi hafanikiwi popote afikapo.] [Twaha: 69].
Asema Sheikhul Islaam Ibn Taimia Mwenyezi Mungu Amrehemu «Hivi ndivyo ilivyo. Hakika ufuatiliaji unaonesha kwamba watu wakitegemea nyota hawafaulu. Si duniani bali vile vile kesho akhera.”
Hayo ndiyo baadhi ya madhara yanayopatikana kutoka kwa waganga waovu.
Kwa hivyo, ni lazima ewe Muislamu kuelekea kwa Mwenyezi Mungu na watu wakumbushane kwamba jambo la kwenda kwa waganga na kuangaliliwa ni jambo baya na halifai. Jueni ya kwamba Mwenyezi Mungu ni Mfalme na Mwenye kumiliki kila kitu, hana wa kumzuwia anapo toa. Ametuamrisha Mola Wetu tutakapo kuwa na tatizo lolote tumuombe Yeye na tumtake Yeye msaada, na yafaa tumtegemee yeye katika kila kitu na tuchukue sababu za kisheria katika kufikia tunayoyakusudia na miongoni mwa sababu hizo ni kumuomba Mwenyezi Mungu dua. Kwa hivyo, atakaemuomba kwa nia njema hakika Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa amali ya anayeomba. Mwenyezi Mungu yuko karibu na hujibu maombi na yeye ndiye anayeruzuku ndege porini na samaki baharini.Amesema Mwenyezi Mungu (Subhanau wa Ta'aala)
اللَّهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَأَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجَ بِهِ مِنَ الثَّمَرَاتِ رِزْقًا لَّكُمْ ۖ وَسَخَّرَ لَكُمُ الْفُلْكَ لِتَجْرِيَ فِي الْبَحْرِ بِأَمْرِهِ ۖ وَسَخَّرَ لَكُمُ الْأَنْهَارَ وَسَخَّرَ لَكُمُ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ دَائِبَيْنِ ۖ وَسَخَّرَ لَكُمُ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ إبراهيم:32-34
[Mwenyezi Mungu ambaye ameumba mbingu na ardhi na ameteremsha maji kutoka mbinguni akatoa kutokana na maji hayo matunda hali ya kuwa ni riziki kwenu na Amewadhalilishia meli ili itembee baharini kwa amri Yake na Akawadhalilishia mito na akawadhalilishia jua na mwezi zinazotembea na akawadhalilishia usiku na mchana na akawapa kila mnachoomba na endapo mutazihesabu neema za Mwenyezi Mungu hamuwezi kuzidhibiti hakika mwanadamu ni dhalimu aliye mkufuru Mwenyezi Mungu. ] [Ibrahiim:32-34]
SIKILIZA MADA HII NA SHEIKH SHADDADI ALI
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.