Menu

Sehemu ya Tarbiya


VIATHIRI AU PINGAMIZI ZA MALEZI


 large 615x330 


Jamii yetu tunamoishi inakabiliwa na matatizo chungu nzima,miongoni mwa changamoto tunazozipata ni kama zifuatazo;
1. Udhaifu wa maarifa na uchache wa elimu
Jambo hili limesababishwa na watu kusoma Qur’an kimajaka pasi na kuelewa tafsiri yake. Watu hawana juhudi ya kuelewa wanayoyasoma katika Qur’an hivyo kuleta ugumu wa kuweza kutumia mafunzo yanayopatikana katika Qur’an kwenye maisha yao. Bali hata ilipopatikana tafsiri ya Kiswahili ya Sheikh Abdallah Alfarsy (Allah amrehemu), ni wachache mno wanaofanya hima ya kusoma tafsiri ya Qur’an. Tatizo hili limekuwa sugu katika jamii zetu hivyo kupelekea ugumu wa kupatikana mabadiliko halisi ya malezi bora. Hii ni kwa sababu, malezi na tabia za Mtume yanapatikana katika Qur’an kwa mujibu wa hadithi ya Aisha Radhi za Allah ziwe juu yake alipoulizwa tabia ya Mtume  akajibu:

 

[فَإِنَّ خُلُقَ نَبِيِّ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيهِ وَسَلَّمَ كَانَ القُرآنَ]      رواه مسلم]

 

[Hakika tabia ya Mtume   ilikuwa ni Qur’an.]   [Imepokewa na Muslim].

2. Kukosekana dira, ratiba na malengo kwa jumla katika malezi yetu.
Malezi yetu yapo katika mfumo wa kubahatisha na kuiga tamaduni za watu wengine wa hususan wamagharibi. Tunawaiga hasa katika mitaala iliyofungamana na taasisi za kikanisa. Pasi na kufahamu tumejikuta ni watu tuliokosa mwelekeo kwa sababu ya kuiga na kufuata mila za watu wengine tukawachana na mila ya Uislamu. Matokeo yake ni kupata vizazi ambavyo viko mbali kabisa na mfumo aliotuletea Mtume wetu .
3. Athari zilizoletwa na mitaala ya shule zinazoegemea sana maono ya kugawanya baina ya dini na dunia.
Mpasuko huu wa watu wanoamini tofauti ya ki manufaa iliyopo baina ya elimu ya dini na dunia imeregesha watu nyuma. Msimamo wa sawa ni kutotafautisha baina ya elimu ya dini na dunia bali mtu awe na yakini ya kuwa elimu yote inatoka kwa Mungu na inapaswa imuelekeze mtu katika kutafuta radhi za Mungu katika maisha yake. Wasioamini msimamo huu umewafanya wakose mwelekeo wa malezi katika jamii.
4. Kutangamana na watu wasio na maadili.
Katika jamii zetu tunatangamana na kuishi na watu aina nyingi wasio na maadili ya kisawasawa. Jambo hili limesababishwa na kugura kwa watu wa sehemu za bara na kuja sehemu za watu wa kwetu kwa malengo tofauti tofauto. Athari za watu hawa waliokuja katika jamii zetu na wenye malengo fiche ,zimeweza kubadili maadili mengi yetu na kuleta ufisadi katika jamii zetu.

5. Falsafa ya uhuru.
Kuna watu wengi wenye msimamo wa kutaka kujikomboa kwa kutumia neno zuri ‘’tuwe huru katika mambo yetu’’ wanataka wafanye wanavyotaka pasi na kufuatiliwa, wasijue kwamba falsafa hii tegemezi yenye asili ya kimagharibi ni sumu iliyotiwa ndani ya asali na sisi pasi na mazingatio yoyote na fikra za kisawa tumetumia sumu hii kiasi cha kutoweza kujinasua hata tukijaribu vipi. Kwa sababu imeingia katika mishipa ya damu yetu na inaendesha maisha yetu.


TANBIHI
Suluhisho ya maradhi haya tuliyoyataja ni kuwa tunahitaji kuja na mfumo mbadala wa taaluma kutokea msingi wa taasisi za mwanzo mpaka ndaki (chuo kikuu), pamoja na kuja na mtaala wenye kuambatana na lengo halisi la dini yetu na kuweza kwenda sambasamba na malimwengu ya kileo.

Makala yameandikwa na: Sheikh Abu hamza

Kusahihishwa kilugha na: Ustadh Ali Juma


Makala yanaendelea



MBINU ZA MALEZI


  mbinu


Malezi  yana mbinu  maalumu  ambazo yataka  tuzifahamu, ili tuweze kuwalea  watoto wetu  kwa njia za kisawa. Mbinu hizi zinabadilika  kulingana  na mabadiliko ya kitaaluma yanavyobadilika kwa kasi sana.Pamoja na  athari ya tamaduni zinazotufikia kupitia mitandao mbalimbali. Kwa hivyo kuna dharura ya kuzifahamu  mbinu hizi haswa ukizingatia kuwa kuna athari  ya utandawazi  katika ulimwengushi  au ulimwengu wa kijiji kimoja.Mambo yafuatayo ni muhimu yazingatiwe:

1.Kwanza mbinu ya kuwa wewe ni kiigizo  chema kwa  namna unavyomlea mtoto au jinsi jamii inavyokutazama  wewe  pamoja na mambo unayoyatenda  kuliko unayoyasema. Kwa hivyo kuwa mfano mwema ni muhimu sana katika malezi.

2.Pili  ni mbinu ya mawaidha mazuri  na kumuelekeza mtoto wako mara kwa mara katika njia iliyonyooka.Kutoa mwongozo wa kimaisha kwa unayemlea ni jambo muhimu sana.Hivi kwamba akue akijua mwelekeo unaoutaka wewe kama mlezi wake.

3.Tatu mbinu ya kumpendezesha  na kumwonesha  uzuri wa lile unalotaka  alifanye, vipi lina athari  na maisha yake na kumwonesha  vipi atafaulu akifuata  yale unayomfahamisha.

4.Nne mbinu ya kumtahadharisha na kumwonesha  madhara na hasara atakazopata katika maisha yake na ubaya wa tabia ile mbaya unayomkataza.Kwa mfano madhara ya kutohifadhi wakati, kukhalifu ahadi, kutokuwa na uaminifu katika maisha yake pamoja na tabia mbaya nyingi.

5.Tano ni mbinu ya kupigia mtoto wako mifano hai  ili aweze kutofautisha baina ya faida na hasara za tabia mbalimbali.Mfano Amati mwalimu mwanachuoni wa kike ambaye mpaka leo yupo katika  uhai na amefundisha  Qur’an miaka 110.Huu ni mfano hai katika nchi ya Kenya mwanamke mshela atumia umri wake wote katika kufundisha dini.Hivi ndivyo jinsi tunavyopaswa kujitolea kwa manufaa ya jamii.

6.Sita ni mbinu ya kutumia  visa vilivyotokea katika kurekebisha tabia fulani. Utoaji wa visa ni mbinu muhimu sana katika kulea mtoto.Kwani waliotangulia walipatikana na mambo mengi ambayo lau watoto wetu watakuwa wakihadithiwa watapata mazingatio mengi sana.Mfano wa kile kisa cha yule mwanamume aliyeuwa watu 99 kisha akarudi kwa ALLAH(S.W.T) kumtaka msamaha.Akakutana na msomi aliyemshauri  atoke katika mji ule anaoishi aende katika mji wa watu wazuri.Kisa ni kirefu lakini faida yake ni kuwa, mwisho ALLAH(S.W.T) akamsamehe.Mazingatio tunayoyapata ni kuwa hatupaswi kukata tamaa na rehma ya ALLAH (S.W.T).

7. Mbinu ya saba ni ya kumzowezesha mtoto kukariri jambo mpaka akazowea  kama alivyofundisha Mtume ﷺ  Swala juu ya mimbari na kama alivyofundisha Sayyidna Uthman b.Affan (R.A) namna Mtume alivyochukua Udhu.Jambo likirudiwarudiwa linabaki kwenye fahamu ya mtoto.

8. Mbinu ya nane ni ya kufaidika na matokeo fulani kisha ukatumia fursa ile kurekibisha kosa au kutilia nguvu fikra fulani kwa kutumia matokeo fulani.Mfano kumsisitiza mtoto afanye bidii ya kuhifadhi Qur’an baada ya kumwona mwenzake akiswalisha msikitini na mengine mengi.  

9.Mbinu ya tisa ni kujaribu  kukuza fikra ya mtoto na kuifungamanisha na utumiaji wa busara katika maisha ya wanadamu.Akue akijua kuwa katika maisha kuna mambo mengi yanayohitaji hekima na busara pasi na kutumia nguvu kukabiliana nayo.

10.Mbinu ya kumi ni kujaribu kukusanya  mazoezi uliyoyapata  kulingana  na tajriba yako katika kutaamaliana  na binadamu wengine.Mtoto wako awe karibu na wewe katika kuona ni jinsi gani unataamaliana na watu.Akiona tabia fulani inajirudiarudia hutakuwa na haja ya kumwambia afanye bali atafanya mwenyewe kwa sababu amekuwa akikuona jinsi gani unavyotaamaliana na watu.

11.Kumi na moja ni mbinu ya kutumia mazungumzo mazuri katika kutafuta usawa wa jambo.Na vilevile kukinaisha watu  katika kutazama mambo na vishawishi tofauti katika maisha.

12.Kumi na mbili ni kujaza nafasi au pengo kwa  kutumia fursa inapojitokeza  au kubuni nafasi ya kurekibisha jambo kwa njia ya hekima na busara.

13.Kumi na tatu ni kuangalia jinsi watu wanavyosuhubiana katika safari na kutazama  vitendo vyao katika safari hizo kwani  mara nyingi watu wanafahamika na kudhirika jinsi walivyo wakati wakiwa kwenye safari.

14.Mbinu ya Kumi na nne ni yakuadhibu  na hii yafaa itumike ya mwisho  baada ya kutofanya kazi mbinu zote kumi na tatu zilizotangulia.Mbinu hii yafaa itumike kwa uwangalifu mno na adhabu iwe ya kipimo na iambatane na kosa mara tu linapofanyika.Kwa mfano ni makosa kwa mzazi kumwadhibu mtoto wake leo kwa kosa alilotenda wiki iliyopita.Changamoto ni kuwa wazazi wengi hawajui mbinu hizi,wao hupindukia katika kutesa na kuadhibu tu.

Hivyo basi ni muhimu sana kuzingatia mbinu hizo ili zirahisishe malezi haswa katika ulimwengu huu wa utandawazi.

Makala yameandikwa na: Sheikh Abu hamza

Kusahihishwa kilugha na: Ustadh Ali Juma

Makala yanaendelea…



MALEZI NA DOTKOMU


 babyoncomp


Sote tunafahamu matatizo yanayo kumba ulimwengu kwasababu ya utandawazi na mrupuko wa maarifa kwa sababu ya mawasiliano yalivyo kuwa rahisi kupitia runinga rununu na mitandao ya wazi. Ni vigumu sana kuhifadhi tabia za watoto katika mazingira haya. 

Tutafanya vipi kama wazazi kuwahami watoto wetu na maafa kama haya.
1. Kuelewa tunaisha katika ulimwengu aina gani na zile biri zinazotukabili katika malezi kila uchao. Kwa kufahamu aina za hatari zilizoko mbele yetu zinazoengezeka kila siku kuwa ulimwengu umekuwa kama kijiji kimoja mila na desturi za watu wengine zinapiga vita maadili ya mazuri ya jamii zetu za kiislamu.
2. Kuweka kinga za kujiepusha na uchafu na fikra mbovu zinazopatikana katika mitandao na kutahadharisha watoto wetu juu ya ubaya unaoletwa na utamaduni huu ya mawasiliano ya teknilojia kuwa rahisi na khatari zake.
3. Kuwa mbadala kwa njia ya kuwashajiisha na kuwafanaya kupenda mazuri yanayopatikana ndani ya hiyo teknolojia na kuwafanya watumie maarifa yale kwa kuboresha tabia njema,kuelimika na kueleimisha wengine. Mfano wa www.eDialogue.org mtandao ambao umewezesha kusilimisha Zaidi ya watu elfu kumi na pia nyaraka wa uso wa kitabu facebook na kiwingu skype na pia nena whatsapp.zote hizi zinaweza kutumika kwa maslahi ya Da'wa.  
a.kueneza Uislamu
b.kuelimisha watu
c.kukataza mabaya
d.kueneza tabia njema
e.kuunga kizazi
f.kuleta umoja wa waislamu
g.kupinga ufisadi
4. kuwepo na ufuatiliziaji na kutathmini miondoko yao ili wasiweze kuchukuliwa na wimbi la ufisadi na fikra potofu na kuingia katika makundi ya kigaidi.
5. Mzazi kuishi ulimwengu wa kileo wa teknolojia ajue yanayoendelea katika mitandao ya wazi kwa mfano facebook uso wa kitabu. Ili aweze kuona mtoto wake anafikiria vipi kuelekea wapi au kushirikiana na kina nani na anasoma nini katika mtandao.
6. Wazazi washirikiane kuanda makongamano ya watoto, safari za pamoja yenye kukusanya mapumziko pamoja na kujitolea kutumikia jamii. Khaswa katika likizo za shule.
7. Mzazi kujua rafiki wa watoto wake kujua wanaenda wapi wanafanya nini na kusoma nini na mipango gani ili aweze kumtahadharisha mtoto na marafiki wabaya.
8. Kuwa karibu na mtoto kwa kuwa rafiki wa mtoto wako na kusuhubiana nayeye kwa kumonesha mapenzi pasina kumnyima uhuru wake kama mtoto.

Imeandikwa na 

Sheikh Abuu Hamza

Mombasa- Kenya.



VIPIMO VYA MALEZI


  educational assessment


Malezi ni nguzo na silaha muhimu sana katika jamii yetu.Hivyo basi tunahitaji vipimo vya malezi ili tuweze kufahamu mwelekeo wa sawa katika malezi yetu. Pasi na kuwa na vipimo hatuwezi kujuwa dira na usawa upo wapi. Je tupo katika njia ilio nyoka ama pana udhaifu? Na kama tumetoka katika dira ya sawa sisi sote tunahitaji kujipima mara kwa mara ili tufahamu kama kweli tumechukuwa mwelekeo wa sawa katika maisha yetu.

Kwa hivyo vipimo tutakavyoviweka ni juhudi za kibinadamu lazima vitakuwa na kasoro zake.Unapoona kasoro yoyote tafadhali tufahamishe ili tujuwe ni wapi pa kurekebisha na malipo yako kwa Mola.
Kipimo cha kwanza ni vipi tutataamaliana na Qurani mwongozo wa maisha yetu? Je mtu afanya mambo yafuatayo?
1-Asoma Qurani kila siku?
2-Ahifadhi kiasi kikubwa?
3-Afahamu maana yake?
4-Azingatia na kufikiria?
5-Aitumia katika maisha yake?
6- Aitukuza Qurani?
7-Ajipamba na adabu za Qurani?
Haya mambo saba ni kipimo cha kila mmoja wetu akitaka kujuwa kuwa malezi yake na watu wa nyumbani kwake wapo katika sawa,basi jipime kwa mizani ya mambo hayo saba.

Mizani ya pili ni hizi hatua saba za sunna za mtume Muhammad (S.A.W).Je watekeleza mambo yafuatayo?
1- Je wasoma hadithi?
2- Je wahifadhi kiasi gani cha hadithi?
3- Je wafahamu maana yake?
4- Je wazizingatia na kuzifikiria?
5- Je wazitumia katika maisha yako?
6- Je waheshimu na kutukuza maneno ya mtume?
7- Je wajipamba na sunna za mtume katika maisha yako?
Kipimo cha tatu kwenye mizani yetu ni je unayo elimu ya kisheria ya kukidhi mahitaji yako ya kimaisha?kwa maana hiyo je una kiwango kizuri cha maarifa au una hima ya kutafuta elimu ya kisheria? Wajua fani za ahkam za ibaada na miamala?Je wajuwa mwongozo wa mtume (S.A.W)?Je una angalau utangulizi muhimu wa fani za kidini kama Tawhid, Hadithi,Sera ya mtume(S.A.W) na fiqhi?Je unaweza kutaamiliana na vitabu vya hadithi na Usulul-Fiqhi? Ukipata majibu ya maswali haya tayari utakuwa umejipima kutumia kipimo cha tatu.
Kipimo cha nne ni kujiuliza je una ufahamu wa kisawa wa ni nani Ahli sunna waa jama’a ?(Wenye kushikamana na sunna na umoja).Mtu Ahli sunna wa jama’a ana sifa zifuatazo;
1 –Anamwabudu Allah pekee yake wala hamshirikishi.
2-Anamfuata mtume (S.A.W) wala haleti uzushi katika dini.
3-Ampenda Mola na mtume wake (S.A.W) kushinda wengine.
4-Aweka mizani baina ya khofu na kutarajia malipo ya ALLAH.
5- Apenda kwa ajili ya Allah na anachukia kwa ajili yake.
6- Anamtukuza Mola wake kila wakati.
7- Anajizatiti sana katika masuala ya tawhidi.
Mizani nyingine ya tano ni ya tabia njema.Je mambo yafuatayo yanapatikana katika malezi ya mtoto wako ?
1- Awe ni mtu anayejipamba na tabia njema .
2- Awe mtu anayeiga tabia za mtume(S.A.W) katika maisha yake.
3- Awe mwenye kuheshimu wazazi wake.
4- Awe mwenye kuheshimu watu wengine wakubwa kwa wadogo
5- Awe ni mwenye kujipamba na adabu za kusema.
6- Awe ni mwenye kujipamba na sifa nzuri.
7- Awe mwenye kujiepusha na tabia mbaya

Mizani nyingine ya tano ni yakufikiria namna yakukuza maarifa ya mtu.Mambo yafuatayo ni ya kuzingatiwa
1-Mtu atumie akili yake vyema pasi na kuishughulisha na upuuzi
2-Mtu akuze maarifa yake mara kwa mara kwa sababu mambo mengi ynavumbuliwa kila siku.
3-Mtu aweze kufanya utafiti wa kielimu kwa sababu yako mengi ambayo yanahitaji masuluhisho.
4-Mtu awe na uhodari wa kufafanuwa mambo kwa uzuri
5-Mtu awe na uhodari wa kuvumbua mambo
6-Mtu ajuwe kutumia vifa vya kileo kama ngamizi (tarakilishi) n.k
7-Mtu aendelee na kuboresha maarifa yake

Mizani nyingine ya saba muhimu ni mizani ya daawah.Katika kufanya daawah mambo yafuatayo ni muhimu sana mtu ayazingatie;
1- Je wafanya daawah?
2- Je wahisi daawah ni jukumu lako?
3- Je wajipamba na sifa za daiyaah?(mwenye kufanya daawah)
4- Je wafuata nyayo za mtume katika dawaah?
5- Je waamrisha mazuri na kukataza mabaya?
6- Je una uhodari wakukinaisha mtu na kumuathiri?
7- Je unaweza kuiendesha idara ya mambo ya daawah ?
Tujipime kwa mizani ya haya tuliyoyaeleza ili tuweze kufahamu kama tupo katika njia iliyonyooka katika malezi yetu na jamii yetu kwa ujumla.
JAZAKALLAH KHEIR


Makala yanaendelea….

Imeandika na Sheikh Abuu Hamza

Mombasa-Kenya.


VIPI TUTAANZA MALEZI BORA KATIKA JAMII ZETU ?


fiches moufid islam 4


Hatua zifuatazo ni muhimu sana kila mmoja wetu azizingatie ili malezi yasiwe ni ya kubahatisha bali malezi yawe ya kitaalamu na kuwe na malengo ya wazi.Kwa hivyo ni muhimu wazazi wasome malezi yenyewe yanavyotakikana Kusomwa. Kusoma vitabu vya malezi na kumsoma Mtume alivyolea watoto wake na alivyofundisha malezi.

1. Kujua namna ya kuchagua mshirika wako katika maisha.Siku zote yataka utazame na kufikiria kuhusu mke au mume mutakayesaidiana naye katika kulea watoto malezi bora.Mtu ambaye mtakuwa na malengo sawa katika malezi ya kufungamanisha kizazi na misingi imara ya Qur’an na Sunnah.

2Kiwango cha maarifa cha mume na mke kiweze kukaribiana ili kuepuka matatizo mbeleni katika kutazama mambo na kuyapima.Mfano viwango vyenu vya masomo viwe vinalingana mfano mwenye shahada ya ndaki na mwenzake awe anakaribia hapo.

3Kuwe na ratiba za malezi na ushirikiano baina ya wanandoa lisiachwe jukumu hili kwa mtu mmoja.Mfano baba akifuatilia masomo basi mama ashughulike kwa kutengeneza mazingira mwafaka ya masomo nyumbani.
4Wazazi wawe mfano mwema kwa watoto wao kwa tabia na wanavyojiweka.Wasitukanane au kutoleana sauti mbele ya watoto wao.Wazazi wawe kielelezo cha kufanya ibada ndani ya nyumba na baba naye ajibidiishe kuswali swala za sunnah ndani ya nyumba yake.Wazazi wasidhihirishe ubaya wao mbele ya watoto.Mfano baba au mama ana udhaifu wa urongo basi asiseme mbele ya watoto au uraibu wa miraa au sigara asiutumie wala kuwatuma watoto.

5. Kuweka vikao vya mara kwa mara vya kifamilia ili kupeana nasiha baina ya wazazi na watoto.Wawashirikishe watoto katika baadhi ya mambo mepesi ya nyumabani na kuwataka ushauri kwa mambo hayo.Kuwasikiliza shida zao na mambo yanayowakereketa.

6Wazazi wawe waadilifu katika kuwapenda na kuwahudumia watoto wao.Wasiwabague watoto katika huduma muhimu kiasi cha watoto wenyewe kujua kuwa fulani anapendwa zaidi na wazazi kuliko sisi.Jambo hili hupanda chuki baina ya watoto na linaweza kusababisha maafa makubwa.

7Kufuatilia tabia za watoto wanapokua katika mabadiliko yanayopatikana katika mwili na hisia.Kuwa karibu nao na kuwapa mwongozo wa sawa kama wazazi.Kuwafanya wajue kuwa lengo si kuwanyima uhuru wao bali ni kuwaonyesha ya sawa ambayo yatajenga mustakabali wao.Mfano kumwamrisha mtoto kuswali anapotimu umri wa miaka saba na kumlazimisha anapofikisha miaka kumi na kumuadhibu anapokataa.Kama alivyo sema Bwana Mtume :

 

 مُرُوا أَوْلادَكُمْ بِالصَّلاةِ وَهُمْ أَبْنَاءُ سَبْعِ سِنِينَ ، وَاضْرِبُوهُمْ عَلَيْهَا وَهُمْ أَبْنَاءُ عَشْرٍ ، وَفَرِّقُوا بَيْنَهُمْ فِي الْمَضَاجِعِ]  صححه الألباني في صحيح أبي داود]

 

[Waamrisheni watoto wenu kuswali wanapofika miaka saba,na muwapige wanapoacha Swala wakiwa na umri wa miaka kumi,na muwafarikishe katika malazi]   [Imesahihiswa na Al-Baniy katika Sunani Abiy Daud]


8. Kuweka risala ya pamoja katika kutekeleza haki ya:

Mwenyezi Mungu Aliyetukuka.
Mtume ﷺ.
Wazazi wawili.
Nasaba yao.
Majirani.
Ummah.
Nafsi.
Haki zote hizi zataka ziwe katika risala ya pamoja wakubaliane kuwa hizi haki zifahamike na zichungwe.


VIPI TUTAWAELIMISHA WATOTO WETU KISAWA ?

Kuwafundisha tawhid nako ni kumpwekesha ALLAH (SWT) na kujitahdhirisha na shirk.
Kuwahifadhisha kitabu cha ALLAH (SWT) kulingana na uwezo wa akili zao.Baada ya hapo ajue maana yake aweze kuizingatia na kuitumia katika maisha yake.Kwa maana hiyo anafaa kuhifadhi,kufahamu,kuzingatia na kuitumia.
Kujua lugha ya kiarabu ambayo ni lugha ya Qur’an na kujifakhiri nayo.
Kumfanya mtume kuwa ndiye kielelezo chema katika maisha ya watoto wetu,kwa kusoma hadithi za mtume na sera yake na kuzifanyia kazi
Kuwaheshimu maswahaba wa mtume wote akiwatanguliza makhalifa wanne Abubakar,Omar,Uthman na Ali radhi za Mungu ziwe juu yao wote.
Kuwafundisha Fiqh ya ibada zake zote,swalaa,Swaum,Zakat na Hajj
kuwafundisha namna ya kufikiria na kupanua uwezo wao wa kutoa masuluhisho.
Baada ya kuweka misingi hii imara unaweza kumpeleka shule yenye nidhamu ili kukuza misingi uliyoijenga.Mfano ni shule za mseto zenye masomo ya dini na kisekula akapate maarifa ya kilimwengu pasi na kusahau akhera yake.

TAHADHARI!!!
UKIWEZA KUJIEPUSHA NA ANASA NYUMBANI KWAKO ITASAIDIA SANA KATIKA MALEZI YA WATOTO WAKO.
JAZAKALLAH KHEIR.

Sheikh Abuu Hamza

Mombasa-Kenya


LOGOISLAM

Search Videos

RSS Content

<

 

WhatsApp This Page Now
 

Visitors Counter

6574386
TodayToday2453
Highest 01-07-2025 : 4073
US
Guests 5

Mkurugenzi na naibu wake

SS10

 

VIKAO VYA OFISI

title_6828e604d9c467919990961747510788
title_6828e604d9d527111725331747510788
title_6828e604d9e698005301741747510788

NISHATI ZA OFISI

title_6828e604db79d3671713701747510788
title_6828e604db8b46660588411747510788
title_6828e604db9c719985728121747510788 Add content here

HUDUMA MPYA

: 4 + 9 =

IslamChoice- Kiswahili

Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi‎ kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.

UongofuUongofu.com