NI MAMBO GANI ANATAKIWA KUFANYA MWANAMKE ALIE KWENYE EDA YAKUFILIWA?
Suala:
Mwanamke aliefiliwa na Mumewe ni mambo gani yanaomlazimu kufanya?
Jawabu:
Ni wajibu kwa mwanamke aliefiwa na mumewe kuomboleza katika muda wa eda , na kuomboleza ina hukmu ambazo ni lazima kuzichunga, tutazifupisha katika mambo matano:
Kwanza : kujilazimisha kukaa katika nyumba yake ambayo anaishi ndani yake wakati wa kifo cha mumewe , hivyo basi atakaa katika nyumba hiyo mpaka kukamilika kwa eda yake ,nayo ni miezi minne na siku kumi kwa neno lake Mwenyezi Mungu aliposema:
[ والذين يتوفون منكم ويذرون أزواجاً يتربصن بأنفسهن أربعة أشهر وعشراً } [البقرة: 234}
[Na wale miongoni mwenu wanao kufa na wakaacha wake, hawa wake wangoje peke yao miezi mine na siku kumi.] [Baqara:234]
Isipokua akiwa mja mzito basi eda yake itaisha pale atakapojifungua kwa neno lake Mwenyezi Mungu aliposema:
[4:وأولات الأحمال أجلهن أن يضعن حملهن } [الطلاق}
[Na wenye mimba eda yao mpaka watakapo zaa] [Twalaq:4]
na hatotoka katika nyumba yake isipokua kwa haja au dharura kama vile kwenda hospitalini kupata matibabu, na kununua vitu anavyovihitaji sokoni kama vile chakula na venginevyo , ikiwa hana wa kumfanyia hivyo.
Pili : Haifai kwake kuvaa nguo nzuri (asivae nguo ambazo zinahesabika ni nguo za mapambo)
Tatu :Asijipambe kwa mapambo ya aina yote kutokana na dhahabu na fedha , na almasi na lulu na mapambo mengine, sawa yawe ni mikufu au bangili au mengineo mpaka eda iishe.
Nne :Asitumie manukato ya aina yeyote sawa yawe Manukato ya kujifukiza au ya Mafuta isipokua atakapojitwahirisha kutokana na hedhi basi itambidi yeye atumie manukato katika sehemu yenye harufu mbaya.
Tano:Asijipambe katika uso wake na macho yake kwa aina yeyote ya mapambo au wanja ,na yale mambo ambayo mwenzako anaweza kukufanyia bila ya wewe kutoka basi mwachie yeye akufanyie ikiwa ukifanya wewe utalazimika kutoka.
Wala hakuna tatizo wewe kuongea na wanaume madamu mazungumzo hayo yapo ndani ya mipaka ya Adabu na heshima , Isipokua makatazo yamekuja katika kulegeza sauti Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema:
[فلا تخضعن بالقول فيطمع الذي في قلبه مرض} [الأحزاب:32}
[basi msiregeze sauti zenu, akaingia tamaa mwenye maradhi katika moyo wake] [Ahzaab:32]
na inapaswa ifahimike yakwamba mazungumzo ya mwanamke na mwanamume inatakiwa iwe katika mipaka ya haja , na jambo hilo halina uhusiano wowote na eda, na ukitokea ukiukaji wowote kutoka kwa mwenye kukaa eda na akafanya ambalo ilimpasa aliepuke basi itambidi aombe msamaha kwa Mwenyezi Mungu na atubie na asirudie tena mambo hayo , na hana kafara isipokua hilo.
Na ALLAH ni mjuzi zaidi
*Chanzo:ISLAMWEB.NET
Imefasiriwa na Mahamd Fadhil El Shiraziy