JE YESU MWANA WA MARYAM ALIKUFA MSALABANI?
Kifo ni jambo nzito mno na halifichiki, wala hutakiwi ujaribu kutoa maelezo ili kudhibitisha eti mungu wako alikufa, kwanza ni aibu na kufru kudai eti aliyekuumba aweza kuuwawa na viumbe vyake, na ikiwa hilo litatokea, basi fahamu moja kwa moja WEWE humuabudu Mola, bali uko katika ibaada ya masanamu au mashetani. Jambo la pili huwezi kutumia maandiko ya Paulo aliyeazimu kwenda kinyume na Nabii Yesu[as] mwana wa maryam, kuwa neon la msalaba kwa wanaopotea ni upuuzi. Hapa bwana watetea kitu Fulani na sina shaka ni mkate wako wakila siku. Qur’aan imesema kuwa kila nafsi itaonja mauti, na kuwa baadhi ya Manabii waliotimilizwa sehemu mbali mbali walipata mateso na wengine wakawa ni wenye kuuwawa. Kwa ayah ii kamwe siyo dalili ya kufa kwa Nabii Issa [Alayhi salaam] mwana wa maryam, bali ni dalili kuwa Bwana Fondo analenga tena kutumia aya zake Allah mtukufu kijanja, na hatuna shaka haya yatamrudi kama yalivyo warudi wale waliofanya azma ya kupigana na Mola na wakashindwa vibaya.
Katika Qur’ani 3:55, Mwenyezi Mungu mtukufu anatupa habari namna wayahood walivyopanga njama za kumwangamiza Yesu, lakini Mola akazipindua hila zao, akamwambia nitakutimizia muda wako wa kuishi, HAWATAKUUA hawa maadui, na nitakuleta kwangu NA NITAKUTAKASA. Waweza kutumia lugha uitakayo, lakini ukweli utabakia, pili neno nitakufisha kilugha katu halina maana ya kufariki dunia, na Yesu [as] asingelisema ‘ waache wafu wazike wafu wao ‘ lakini najua hiyo kwako ni fikra ngumu.
Qur’ani imetoa msimamo mmoja kuwa Nabii Issa Yesu [Alayhi salaam] hakufa kamwe msalabani kama wanavyodai wenyekujitafutia katika Qur’ani 4:156-158.
[Na pia kwa kufuru zao na kumsingizia kwao Maryamu uwongo mkubwa.Na kwa kusema kwao: Sisi tumemuuwa Masihi Isa, mwana wa Maryamu, Mtume wa Mwenyezi Mungu - nao hawakumuuwa wala hawakumsalibu, bali walifananishiwa tu. Na hakika walio khitalifiana katika haya wamo katika shaka nayo. Wao hawana ujuzi nayo wowote, ila ni kufuata dhana tu. Wala hawakumuuwa kwa yakiniBali Mwenyezi Mungu alim- tukuza kwake, na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.]
Wayahood walidhani Nabii atakae tumwa kwao atawaongoza katika vita dhidi ya warumi waliokuwa wakiwatawala zama hizo, lakini kinyume chake akawa mpole na kulipa ushuru kwa warumi, hili liliwafanya wayahoodi waanzishe fitina nyingine ambayo ipo hata leo kuwa Mama Maryam alifanya uchafu ili azaliwe Yesu [Alayhi salaam] Hii ndio sababu yao kupanga njama za kumuangamiza.
Biblia imeandikwa na hao waandishi kuwa kila mwenye madhambi makubwa kama ubakaji, mauaji yasiyo ya haki, hukumu yao ni kuuwawa kwa kusulubishwa, katika Torati 21:22, vipi huyu unaye muita mungu wako afe kifo cha fedheha?, ikiwa Yesu [as] hakutenda dhambi niwazi kuwa hakufa msalabani, na kama tulivyo bainisha, kwanini adhulumiwe?
Wako wakristu wengi wasio jua kuwa msalaba ni chombo kitesi, na misalaba ilikuweko miaka mingi kabla hajazaliwa Yesu [as] mwana wa maryam, na katika Tourati aliyo pewa Nabii Musa [Alayhi salaam] kuwa kila aliyeangikwa msalabani amepata laana yake Allah [swt], nasi waislam katu hatukubali Nabii Issa [Alayhi salaam] aliingizwa katika laana kama anavyodai bwana Fondo na wote wenye fikra kama yake, lakini vipi afe kifo hicho cha laana hali yeye ndiye mungu kwa wakristu!. Kwa nini sisi tujiingize katika hali ya kutatanisha na kujaribu kutoa sababu zetu wenyewe zisizo kuwa na msingi wowote.
Ndugu wasomaji ni Qurani pekee iliyo simama kidete katika kufahamisha ukweli ambao umefichwa kwa miaka mingi kuwa Yesu [as] hakufikishwa msalabani, na kuwa msimamo huu umebakia katika hali hiyo hiyo kwa takriba miaka 1438, kinyume na vitabu vingine ambavy hubadilishwa kila uchao, na kwake kudai kuwa Biblia yote ni maandiko yake matakatifu ni uwongo wa hali ya juu kwa mtu huyu anaye tafuta umaarufu, na makasisi ishirini na tisa kati ya makasisi thelathini na moja wa Uingereza wamekiri kwamba Yesu [as] kweli aliishi humu duniani, lakini kwamba alisulubiwa ni uwongo wa kujitafutia maslahi. Mgongano ulioko kwenye Biblia ni wakutishia, mfano alivaa nguo rangi gani nyekundu au zambarau, alisulubiwa saa tatu asubuhi au saa tisa?
Kando na migongano tuliyo nukuu hapo, bado utaona utata wa wale waliokwenda kaburini kungali asubuhi ili ‘kuupaka’ mwili wake mafuta walikuwa wangapi, mfano:-
1.Mathayo 28:1-2--wanawake wawili [2] tu ndiyo walio kwenda kaburini, Mariam Magdalene na mariam wa pili.
2.Marko 16:1-3--waliokwenda kaburini ni Mariam Magdalene, Mariam mamaye Yakobo, na Salome [3]
3.Luka 24:1, 10—waliokwenda kaburini alfajiri ni wengi tu sana, mariam Magdalene, na Yoana, mariam mamaye Yakobo, na wale wanawake wengine!
4.Yohana 20:1—Aliyekwenda kaburini ni mmoja tu naye ni Mariam Magdalene.
Nani awezaye kuamini mambo haya yasiyoelekea, lipi la kuaminika katika vitabu hivi vinne visivyoelekea, kasha tudai kutafuta mwongozo wa kisawa. Jambo linguine la ajabu ni kuwa kwa taratibu na mila za wayahood wanawake katu hawaendi makaburini, wala haijatokea kuwa maiti aliye zikwa siku tatu aweza fukuliwa tena ili maiti apakwe mafuta, lakini kwenye Biblia ambayo Fondo angependa tuiamini imeandikwa hayo ya yakuchekesha.
Katika Mathayo 27:62-66, Nabii Yesu [as] mwana wa Maryam ameitwa mjanja!, na juu ya yote wakasema kuna uwongo ule mwisho utapita ule kwanza, ajabu hata leo wasomi katika ukristu hawataki kueleza maneno hayo. Mara nyingi utaona kuwa ndugu Fondo anadumu katika kutoa maelezo yake ili kujaribu kufidia pale anapodhania kuwa kuwa anavyofikiri, amekuwa mhariri wa Mwenyezi Mungu!
Tangu jadi kuna madhambi ambayo waja wanatoa kafara kwa kuchinja mnyama ima kondoo, ngombe, mbuzi au ngamia, na sio lengo kuwa mnyama mmoja asafishe madhambi ya watu wote kama anavyofikiri Bwana Fondo na angependa sote tuwe kama alivyo jambo ambalo haliwezekani kamwe.
IMETAYARISHWA NA :
ADAM AMBETSA
MWEMBE TAYARI TABLIGH GROUP
MOBILE NO. 0723 17 41 54
MOMBASA, KENYA.
JE UANA WA YESU UNAOKOA?
Mwenyezi Mungu Mtukufu ameeleza katika Qur'ani kuwa asili ya itikadi kuwa Mola ana mwana ni itikadi ya wayahood wakadai kuwa Uzair ni mwana wa Mwenyezi Mungu
[Na Mayahudi wanasema: Uzeir ni mwana wa Mungu. Na Wakristo wanasema: Masihi ni mwana wa Mungu. Hiyo ndiyo kauli yao kwa vinywa vyao. Wanayaiga maneno ya walio kufuru kabla yao. Mwenyezi Mungu awaangamize! Wanageuzwa namna gani hawa!]
[Quraan 9:30].
Katika Quraan 2:116, Mwenyezi Mungu Mtukufu anawarudi mayahoodi na wakristu kwa madai yao kuwa Allah Subhanahu wata'ala ana mwana akasema:
[Na ati wanasema: Mwenyezi Mungu ana mwana. Subhanahu! Ametakasika na hayo. Bali vyote viliomo mbinguni na duniani ni vyake. Vyote vinamt'ii Yeye.]
Huu ni ushirikina mkubwa , kila unachokiona na usichokiona vyote vina mtii Yeye kwa unyenyekevu, na Mtume Rehma na amani zimfikie yeye akasema kupitia hadith aliyoieleza ibn Abbas, kuwa Allah Mtukufu amesema Mwana wa Adam anasema uwongo dhidi yangu, japo hana haki kufanya hivyo, ananitukana Yakuwa hana haki ya kufanya hivyo. Kwa kusema uwongo dhidi yangu husema kuwa siwezi kumuumba tena alivyokuwa baada ya kufa, na kwa kunitukana ni kule kuwa nina mwana, la ametukuka! Hana mke au mwana’
Napenda sana kuwajulisha wasabato na wakristu kwa jumla kuwa usitafute sababu yoyote ili Mola awe na mwana, huo ni upagani ulio wazi, na moja katika sababu kubwa ya Allah Subhanahu wata'ala kuiteremsha Qur'ani ni kuwaonya wale wanaodai Mola ana mwana wao hawana ilmu au baba zao na hawasemi ila uwongo, na fondo ni mmoja wao, Qur'ani 18:4-5. Kwa nini kujisumbua kama uana uutakao wewe ni wa kizazi au heshima. Kwa Allah Subhanahu wata'ala sote ni viumbe vyake tu [Isaya 44:24], Fondo wajisumbua sana eti ALIYEZALIWA na mungu hatendi dhambi. Malaika wote hawatendi dhambi na wala hawajaitwa watoto wa mungu. Usiweke vigezo vya kutafuta muradi wako. Kwamba Yesu Alayhi salaam mwana wa maryam ni mtakatifu siyo hoja haswa kwa wakristo kwa kuwa Mathayo,Marko,Luka na Yohana wote ni watakatifu, na Pope pia ni mtakatifu!.
Bwana Fondo anafanya ubaguzi, Daudi Alayhi salaam aliongea kwa uwezo wa roho mtakatifu na hakuitwa mwana wa mungu, na kuhusu ushahidi Mola ni shahidi tosha wala hatuhitaji mwingine, na juu ya hayo na watu watakao dai madai kama ya Fondo watakuwa wamefeli, na kujiingiza katika ushirikina ulio wazi.
Katika utafiti ambao tumefanya unatuonyesha kuwa Yesu Alayhi salaam mwana wa maryam alijiita mwana wa Adam mara themanini na tatu [83], lakini kaitwa mwana wa mungu na hawa wapotofu mara ishirini na nne [24] tu!. Jee una lengo lipi kama huwezi waambia wafuasi ukweli huu?.
Kwa wasomi wa Qur'ani, mtagundua kuwa Mwanamke aliyetajwa kwa jina katika aya za Qur'an, ni mwanamke mmoja tu nae ni Maryam binti Imran, soma katika sura ya kumi na tisa [19].
Mama huyu Allah Mtukufu kamtaja kwa jina na kumueleza kwa undani kwa sababu ndiye alomzaa Nabii Issa Alahyi salaam (Yesu) mwana wa Maryam ambaye baadhi ya wakristu wamemuita Mwana wa Mungu, na wengine kudai ndiye Mungu haswa!. Sisi kamwe hatujengi hoja kwa sura ya Qur’ani 112:1-3, kwa kuwa muradi wa aya ni Tawheed yaani kumpwekesha Mola, kumtakasa, cheo chake,uwezo wake ,utajiri, uumbaji wake na kuwa hakuna mwenginewe ila Allah Mtukufu, na haya ni majibu yake Allah Subhanahu wa Ta'ala kwa wale waliotaka kujua hakika ya mambo.
Mwenyezi Mungu Mtukufu ni muumba, na sifa ya kuza ni ya majini, wanadamu na wanyama Mwenyezi Mungu mtukufu amekamilika kwa hali ya kipekee.
Fondo na baadhi ya wakristu wanashangaa kwa nini mbingu hazitatuki, na milima kuwa kama sufi kama ilivyoeleza Qur’ani, ukweli ni kwamba Rehma za Allah zimetangulia Hasira zake, na waswahili walishasema ‘ aulizae atapata ‘. Kwa kudai madai haya Fondo amedhihirisha ukafiri wake, na Maana haswa ya ukafiri ni kukanusha haki,kuficha haki na kuikataa haki. Kufanya kibri kwa maneno yake Allah Subhanahu Wata'al, ni hatari kubwa sana ambayo Fondo na wakristu wenzake wanafanya, na ni fikra za kijahiliya na ni dalili ya kutokuwa na ilmu kwake na babu zake na ni upotofu uliodhahiri.
Allah Subhanahu Wata'ala, ametuonya sana kuepukana na uzushi, na kama angekuwa na mwana angelibainisha katika vitabu, na Manabii wala asingetuacha kuwauliza wasiokuwa na ilmu kama ndugu zetu. Kwamba Nabii Isaa Alayhi salaam (Yesu) Mwana wa Maryam hana Baba, haimfanyi awe mwana wa mungu au mungu, na kuwa fikra au imani hiyo ni upotofu na hauna faida yoyote ikiwa mja hatamwabudu Mwenyezi Mungu Mtukufu kama ilivyonukuliwa katika Mathayo 4:10, Yohana 14:1-, na Yohana 17:3. Jambo la pili ni kuwauliza ndugu wakristu, Nabii Adam Alayhi salaam hana baba wala mama, lakini hajaitwa mwana wa mungu au mungu, na ndio twasema kuwa hao wanaotangaza upotofu huu ni lengo la kufaidika kibinafsi, wala sio kuelekeza watu katika uzima wa milele.
Ni makosa kwa Bwana Fondo kutumia janja kugeuza au kuficha mashetani wanao kizazi kwa kuwa wanazaana, Allah Subhanahu wa Ta'ala ni muumba na hana watoto, lakini kwa bwana Fondo ili afikie faida yake ya binafsi lazima ageuze aya ya Qur’aan 2:116, anapodai kuwa Qur’ani inakubaliana na fikra hii ya kijahiliya.
Katika Kumbukumbu La Tourat 32:39-40, Mola anajitukuza mwenyewe kuwa ndiye anayeuua na ndiye pekee anayeweza kuweka hai, ndiye anayejeruhi na kuponya na pekee tu ndiye MWOKOZI, leo kwa bwana huyu kudai kuwa uana wa Yesu Mwana wa Maryam unaokoa ni wazi haelewi anachozungumzia, na cha maana kwake ni apate muradi wake tu.
IMETAYARISHWA NA :
ADAM AMBETSA
MWEMBE TAYARI TABLIGH GROUP
MOBILE NO. 0723 17 41 54
MOMBASA, KENYA.
JE YESU NA ISSA (A.S) NI MTU MMOJA?
Mwanadamu anapoongozwa na uoga, mara nyingi hutoka katika mipangilio sahihi
na kuchukua muda wake mwingi akijaribu kubuni njia na mikakati ya kumkinga
asipoteze alichonacho na waliomzunguka. Kwa hivyo hujifanya kama ni tofauti na
wale wanaomsikiza kiakili, katika kuelewa na kwa njia hii hubuni uwongo wa
kumdumisha katika biashara ya pekee anayoijua yeye.
Waislamu hatukuamriwa kudharau, kuchukia au kubagua mtu yeyote kwa misingi
ya rangi, awe mke au mume kuwa tukuza Manabii hadi kiwango cha kusema
ili kujifurahisha tu kwa muda kuwa Yesu, Issa na Jesus ni watu tofauti, bali Quran
imetuamuru hivi:
“Sema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu, na tuliyoteremshiwa sisi, na
aliyoteremshiwa Ibrahim na Ismail na Is-hak na Yaqub na wajukuu zao na
aliyopewa Musa na Issa na Manabii wengine kutoka kwa Mola wao. Hatubagui
baina yao hata mmoja na sisi ni wenyekevu kwake.” (TMQ 3:84)
Sisi waislamu hatuna tabia ya baadhi ya wakristo kubagua Manabii, bali
tunawaamini, kuwataja kwa heshima yao pamoja na kuwahami kutokana na wale
ambao wana itikadi mbaya. Lakini kila wakati waislamu wanapokuja pamoja ili
waishi kwa undugu wa kibinadamu na wakristo, wako wanaotafuna changarawe
za fitna eti Yesu, Issa na Jesus ni watu tofauti!
Katika kurasa hizi hatulengi kuunga wala kupinga wale wakristo wanaosema Yesu
mwana wa maryamu ndiye mungu, mwana wa mungu au zote (mungu tena
mwana wa mungu) bali ni kukupeni mwelekeo ulio sahihi kwa atakaye maana,
hakuna kulazimisha mtu katika dini (Quran 2:256)
Ulimwengu umeweka vitu vinavyoitwa International Standards na huwezi kuleta
chochote kinyume chake, na kuwa umekileta na kinatumika sio dalili kuwa uko
sawa, bali wale waasisi wa ubaya huo wanafurahi kukuona ukididimia kwenye
lindi la upotovu.
Ni habari za kuaminika kuwa kuna vitu vinne kisheria ya uandishi havifanyiwi
tafsiri na utaona katika ramani ya biblia yako jina la mto Yordani halijafanyiwa
tafsiri, mto Nile, Tigris, Euphrates na mingineyo imebakia na jina asilia. Jina la
mto au jina la nchi, jina la mtu au mlima haliwezi kufanyiwa tafsiri lakini kwa
hawa ndugu wakristo katika Biblia yao majina ya watu yamefanyiwa tafsiri eti
Yesu ni Kiswahili na Jesus ni Kizungu lakini lugha yake ya asili usiijue?
Wengi hawajui kuwa jina “Issa” ni jina la ki israeli na kama waeza kufuatilia hebu
tafuta maana na namna jina hili linavyosomwa “ESSAU” na sina shaka utafahamu
Kwa sababu ya kudumisha utengano na maelewano, sote twajua kuwa “Issa”
ndiye huyo “Yesu” kama vile mkate ndio “Bread”
Quran na Biblia zimetuonyesha kuwa Mama Maryamu a.s. alizaa mtoto wa
kiume aliyetahiriwa siku ya nne kama ilivyo desturi ambaye alitukuzwa mno na
Mola s.w.t.
1. Quran 3:45 – Malaika waliotumwa kwa Mama Maryam.
2. Luka 1:26 – Mwezi wa sita Malaika Gabriel alitumwa kwa Maryam.
3. Quran 3:47 – Maryam ni Bikra hajui Mume.
4. Luka 1:34 – Maryam ni bikra hajui mume.
Quran inamtambua Yesu kuwa ni mwana wa Maryam sawa na andiko la Biblia,
sasa vipi mtu aseme Yesu na Issa ni tofauti?
1. Quran 3:45 – Jina lake ni Issa mwana wa Maryam.
2. Marko 6:3 – Yesu, mwana wa Maryam.
Kuna katika wakristo wanaodhani kuwa kwa mujibu wa Quran mwana wa
Maryam hakufanya miujiza na wakawadanganya wakristo hivyo lakini Quran
yaonyesha baadhi ya miujiza yake japokuwa wanadamu hawataki kuukubali
1. Quran 3:49 – Isa mwana wa Maryam aliwaponya baadhi ya vipofu, wenye
ukoma, na kufufua baadhi ya waliokufa kwa idhni ya Mwenyezi Mungu.
2. Yohana 11:38 – 44 – yesu amuomba Mwenyezi Mungu amfufue lazaro ili
wale wa Izraeli wajue kuwa Yesu alitumwa na Mungu. Kando na kumfufua
Lazaro, aliwaponya viwete, vipofu, mabubu n.k.
Ili kutukinga na shirki, Quran ikatuonyesha kuwa mfano wake Yesu ni kama Adam
a.s. wote waliumbwa kwa udongo na Mola s.w.t na hawastahiki kuabudiwa kwa
vyovyote na yeyote.
1. Quran 3:59 – Issa ana asili kutokana na Adam.
2. Mathayo 26:64 – Yesu ni mwana wa Adam.
3. Mathayo 19:27 – Yesu ni mwana wa Adam.
Kihakika ni masikitiko kwa baadhi ya wakristo kudai leo eti wa Izraeli hawamjui
Yesu ilhali Maryam aliyemzaa ametokana na wana wa Izraeli. Sasa wewe mkenya
utamjua Yesu kulikoni mama yake?
1. Quran 3:49 – Issa ni mtume kwa wana wa Izraeli tu.
2. Quran 61:6 – Issa ni mtume kwa wa izraeli tu.
3. Mathayo 10:5 – Yesu atuma wanafunzi wake kwa kabila za wa Izraeli.
4. Mathayo 10:23 – Wao wanafunzi hawataimaliza miji ya Izraeli
5. Mathayo 15:21 – 26 – Yesu ametumwa kwa wa Izraeli pekee.
6. Matendo 2:22 – Yesu amedhihirishwa kwenu (Waizraeli) na Mungu.
7. Matendo 5:31 – Yesu ameleta toba kwa waizraeli tu.
8. Matendo 11:19 – wanafunzi walifundisha habari za Yesu kwa waizraeli tu.
9. Yohana 17:9 – Yesu anawaombea hao, haombei ulimwengu.
Kama “Issa”, “Yesu” naye hawezi kuokoa na hajui siku ya Qiyama na hawezi
kufanya lolote ila aamriwe na Mungu.
1. Quran 31:34 – habari za kiama ni zake Mola tu.
2. Taurati 32:39 – Mwenyezi Mungu tu ndiye anayeokoa.
3. Yohana 5:30 – Yesu hawezi kufanya lolote ila aamriwe.
4. Mathayo 20:20 – Yesu asema uzima wa milele watapewa waliowekewa
tayari na Mola.
5. Yohana 14:28 – Mungu ni mkuu kuliko Yesu mwana wa Maryam.
Quran imesimama msimamo mmoja na ndio mwafaka wa jamhuri ya Maulamaa
kuwa mwana wa Maryam hakufa msalabani.
1. Quran 4:157 – hakufa msalabani, ila wao wanafuata dhana.
Ikiwa Yesu alikufa msalabani na ndiye Mungu wa baadhi ya wakristo basi
yasikitisha kwa kuwa yaonyesha udhaifu wa Mungu huyu hata auwawe na viumbe
vyake. Kwa hakika maandiko ya Biblia yameachana sana kuhusu kifo cha Yesu
msalabani na ni vigumu kwetu kuamini na mifano ni mingi tu: -
1. Mathayo 27:27 – Yesu kavishwa vazi jekundu.
2. Marko 15:16 – Yesu kavishwa vazi la rangi ya zambarau.
3. Marko 15:25 – saa tatu asubuhi Yesu amesulubiwa.
4. Yohana 19:14 – Saa sita Yesu yuko mahakamani.
5. Mathayo 27:3 – 5: Je Yuda alijinyonga?
6. Matendo 1:18 – 20: Au Yuda alianguka akapasuka tumbo?
Ikiwa wafuasi wa Yesu ni wakristo (Christians) Je Yesu mwenyewe alikuwa na dini
gani na je jina la mtu laweza kuwa dini ya watu?
1. Quran 61:14 – Mtume Issa alikuwa na wanafunzi wake.
2. Mathayo 10:2 – Majina ya wanafunzi wa Yesu.
Kama ni kweli kuwa Yesu aliyezaliwa na Maryam ni Mungu na kuwa anao ndugu
zake kama munavyotuonyesha basi mna bahati kuwa mungu mwenye ndugu na
ukoo. Sisi waislamu hatuna.
Mathayo 1:1
Uislamu umetuonyesha kuwa baada ya kumzaa “Issa”, Maryam hakuolewa,
hakuingiliwa na mtu yeyote hadi alipokufa, yaani ndiye mwanamke pekee aliyezaa
pasina kuingiliwa na akafa bila kuingiliwa.
Yesu alifundisha njia ya Mungu akisema “utuongoze katika njia iliyonyooka.”
1. Mathayo 6:9
2. Luka 20:21
Kasema kuwa kuna utatu ni kumtukana Mola, ni kumtukana Nabii Yesu, Yesu ni
mtume tu.
1. Yohana 17:3
2. Yohana 5:30
3. Yohana 7:16 – 18
4. Marko 12:28 – 31
5. Mathayo 4:10 – “Huo utatu watoka wapi hali Yesu mwenyewe
alimuabudu Mola, vipi wewe unamuabudu Yesu na udai kuwa Nabii Isaya
alihakikisha, hali Isaya alisema “tumepewa mtoto mwanamume” vipi
Mungu awe mtoto tena wa “kiume” kumbuka kuwa Mola hana mfano
wowote.
Yesu mwenyewe alisema waache wafu wazike wafu wao, tena angoje wafe ili
awahubirie, kuongea na wafu huu si ushetani!utafute jina Issa kwa Biblia na hao
waandishi wa biblia wamesema katika dibaji ya union version 1952 kuwa:-
…Hio kazi yenyewe haikuwa rahisi. Matumizi mbali mbali yametokea katika
Janibu mbali mbali za nchi hii. Kwa mfano ilikuwa hapana budi kufikiri kwamba
hilo jina la Mungu katika agano la kale litaandikwa “Jehova Mwenyezi Mungu
au Bwana Mungu…pia maendelezo ya majina yote ya watu nay a mahali ilikuwa
lazima yafikiriwe tena na mengine kutengenezwa. Jambo hili lilikuwa kazi
kubwa sana kwa sababu yako majina zaidi 3500. Tena jina la kitabu chenyewe
lilifikiriwa, kama kiitwe “Maagano mapya” au agano jipya.
Ndugu msomaji, bado wataka kuona neno “Issa” katika Biblia? Hizi ndizo taratibu
ya Iman kama ilivyoeleza Quran:
“Hiki ni kitabu kisichokuwa na shaka ndani yake, ni muongozo kwa wacha
Mungu ambao huyaamini mambo ya ghaib na hudumisha sala na hutoa katika
vile tulivyowapa.” (TMQ 2:2 – 3)
Naye Yesu akasema:
“si kila mtu aniambiaye Bwana, bwana, atakayeingia katika ufalme wa
mbinguni, bali ni Yule afanyaye mapenzi ya baba yangu aliye mbinguni.”
(Mathayo 7:21)
Amua, utamuita “Yesu simba” au utafanya mapenzi ya Mungu?
Imetayarishwa na
Adam Ambetsa
Tel No: 0723 – 174 154
Mombasa.
MAJIBU KWA BWANA FONDO NA WASABATO KWA JUMLA
Bwana Fondo, kijana wa kisabato [SDA] anapenda sana aitwe “Ustadh”, na ndivyo wanavyotaka wahubiri wote wa kisabato, lakini ni mapenzi tu wala haimgeuzi kuwa anavyotaka kwa kuwa mtume [Rehma na amani ziwe juu yake] asema Imani haiji kwa kutamani. Hatujapenda sana kuwajibu hoja zao zisizo kuwa na kichwa wala maguu, lakini kwa hili tutajaribu kuuzuia huu utapeli wa maandiko yake ili apate muradi wake. Hatuzuii haki yako kupata riziki, lakini ziwe ni za halali.
Katika kijitabu alichoandika kina mada tano kimsingi, na zote amezipinda ili zimfae binafsi, na kuwapotosha wanaokisoma hali hawana ujuzi, mada hizo ni:-
1.JE NI UPI MWONGOZO WA KWELI, BIBLIA AU QURAAN.
2.JE UANA WA YESU UNAOKOA.
3.JE YESU ALIKUFA MSALABANI.
4.JE NANI MWOKOZI WA ULIMWENGU MZIMA, MOHAMMAD[SAW] AU YESU.
5.JE NI IPI NJIA YA KWELI YA UZIMA, UKRISTO AU UISLAMU.
Tutajaribu kuiangazia kila mada kwa undani kidogo kwa kutoa baadhi ya maandiko ambayo Bwana Fondo hakutaka ujue kwa sababu zake, lakini ndugu msomaji yafaa ujue agano la mwisho, Qur'ani ilikwisha twambia ukweli umeshafika na uwongo lazima utoweke [Quraan 17:81], na sina shaka kuwa hata yeye mwenyewe ajua hayo aliyoyaandika si kweli.
Mada yake ya kwanza ni, JE NI UPI MWONGOZO WA KWELI, BIBLIA AU QUR'ANi?
Kosa lake la kwanza ni kule kujifanya kuweza kusoma anavyofikiri Muislam, na kuzua uwongo unaoendelezwa kuwa Waislamu hawakusoma, kwa hivyo hujipangia mambo bila dalili maalum kutoka kwa Allah [Subhana wata'ala], hii si kweli, bali kinyume chake Uislamu ndio Dini pekee duniani ambayo ambayo viongozi wake wamesoma na kumjua ALLAH [Alayhi Salaam] namna inavyotakiwa , na hawatowi hutuba zao ila zina ushahidi kamili wa Qur'ani na Hadith za Mtume [Rehma na amani zimfikie yeye], kinyume na madini mengine ambayo viongozi wake hudai eti wamefunuliwa na kufungua majumba ya ibaada!.
Hakuna ushahidi wowote kuwa Mwenyezi Mungu aliteremsha au kumfunulia Nabii yeyote kitabu kiitwacho BIBLIA, na wala Waislam hatusemi kamwe kama anavyodai Fondo, kuwa ni BIBI-LIA, bali twajua kihakika kuwa Mola Muumba aliteremsha Tourati kwa Nabii Musa [Alayhi Salaam], Zaburi kwa Nabii Daud [Alayhi Salaam], Injeel kwa Yesu [Alayhi Salaam] mwana wa Maryam na Qur'ani kwa Mtume Muhammad [Rehma na amani ziwe juu yake]. Haya maelezo ya Biblia yanayotolewa na bwana huyu yana mkanganya yeye mwenyewe. Neon Biblia asili ya kigiriki, BIBLOS, na maana yake ni Mkusanyiko wa vitabu, hapa lazima tuzingatie mno kuwa haikuja ‘ mkusanyiko wa vitabu vya Mola’, na kwake kujaribu kunukuu maandishi ya Biblia ya Union Version iliyoandikwa 1952, eti maandiko ya Mungu yaitwayo Biblia yaliyongezewa na waandishi kujaribu kuziba mapengo na mapungufu katika kitabu hicho chao ni uwongo wa ajabu.
Kwa wale wanaokikubali kitabu cha Biblia kuwa kitakatifu, ilikuwaje wagiriki ambao kiasili ni mapagani wawe ndio watakipeni jina kitabu chenu?, hakuna nabii mgiriki, kwanini Biblia ya kwanza iwe ni ya kigiriki?, unaposema eti Mungu aliwapa wakristu kitabu kilichokusanya vitabu manabii walio tangulia ni mawazo tasa, na ya uvunjivu mkubwa wa Haki yake Mwenyezi Mungu, na sina shaka kesho ataulizwa ni Nabii yupi aliye pewa kitabu cha Biblia?. Aya aliyoitoa ya Qur'ani 2:121 yasema hivi, ‘ wale katika ahlul kitabu, tuliyo wapa kitabu, tourat, Zaburi na Injeel, wakakisoma kama ipasavyo kukisoma bila ya kupotoa tafsiri, kwa kuongeza hili au kupunguza hili hao huiamini hii Qurani wakasilimu’, lakini Fondo kaamua kucheza na akili za wasabato kwa kujivika kofia ya UANDISHI, kumbe katu hayumo.
Qur'ani haikuja kijanja, na kamwe haifai kutumiwa kijanja. Waislam sote tumelazimishwa kuwakubali Manabii wote aliyo wataja Allah Sub'hanahu Wat'ala katika aya kadhaa za Qur'ani, mfano [2:136,]
[Semeni nyinyi: Tumemuamini Mwenyezi Mungu na yale tuliyo teremshiwa sisi, na yaliyo teremshwa kwa Ibrahim na Ismail na Is-hak na Yaakub na wajukuu zake, na waliyo pewa Musa na Isa, na pia waliyo pewa Manabii wengine kutoka kwa Mola wao Mlezi; hatutafautishi baina ya yeyote katika hao, na sisi tumesilimu kwake.]
na [3:84]
[Sema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu, na tuliyo teremshiwa sisi, na aliyo teremshiwa Ibrahim, na Ismail, na Is-haak na Yaakub na wajukuu zao, na aliyo pewa Musa na Isa na Manabii wengine kutoka kwa Mola wao Mlezi. Hatubagui baina yao hata mmoja, na sisi ni wenye kusilimu kwake]
na zingine nyingi zinazowaamuru waislam kuwapa heshima na kuwahami Manabii wote waliotajwa.
Ibraheem [Alahi salaam] hakuwa myahoodi wala mkristu bali alikuwa mwongofu mtii wala hakuwa miongoni mwa washirikina, Waislamu tunamtambua kama Baba wa Mitume na Baba wa Imani, na wanawe wawili Nabii Ismail [Alahi salaam], na Nabii Isaack [Alahi salaam] ambao wote Allah [Subhana wata'ala] aliwajaalia kuwa Manabii watukufu. Kasha kuna Nabii Yakoob [Alahi salaam] na kizazi chake [Banu Israel], na aliyopewa Nabii Musa [Alahi salaam], na Issa Yesu [Alahi salaam] Mwana wa Maryam ambao ni ujumbe mtukufu kwa wana wa Israeli tu wala si kwa watu wengine [ambao ni watu wa mataifa wasiyo tahiri].
Anapouliza ndugu yetu Fondo, nani walioandika Biblia, kisha akatoa andiko la kutoka 31:18, torati iliandikwa na chanda cha Mungu, na hapo hapo akageuza hapo ili kuleta dhana kuwa mwandishi wa biblia ni Mungu ni kumsingizia Mola uwongo, tena uliyo dhahiri, na mwanadamu aliye fikia kiwango cha kusema uwongo juu ya Mwenyezi Mungu huwa kavuka mipaka yote, na ameanzisha vita na Mola wake nasi hatuna shaka kuwa atashindwa vibaya sana .
jambo linguine la kudhibitisha alikuwa hamaanishi kwa yale aliyo andika , ni matumizi ya N/B. Hii inampa nafasi ya kuongeza au kupunguza yale atakayo ili apate muradi wake. Waislamu twajua kuwa asili ya ilmu zote ni Allah [Subhana wata'ala], kama alivyo sema mwenyewe katika Qur'ani [96:1-5,]
[Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba,Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote!Ambaye amefundisha kwa kalamu.Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui.]
na katika ilmu hizi zote ni za uhakika, lakini pindi mwanadamu atakapo kuanzisha kidini chake au kujitukuza mwenyewe, basi aya zote hizi huzigeuza sharubati ili apate utamu wa dunia,atambuliwe, apate cheo kuwa huyu ndiye mpinzani mkuu wa Mola, lakini angalia mwisho wa Firaun [aliye laaniwa].
Kile Fondo anawaficha wasabato wenzake na wakristu kwa jumla ni kuwa Biblia ina mamia ya waandishi walioiandika zama hizo, kama vile Luka aliyekuwa mganga [upo ushahidi wa biblia ya Imprimatur Bible], Paulo [zamani akiitwa saulo] aliyeandika nyaraka nyingi mno katika biblia, [filemoni 1:19] , na hata lile koti [joho] alilolisahau huko troa akaomba aletewe, na bado yakaitwa ‘ maandiko matakatifu ya mungu yaitwayo biblia’. Kufikia hapa napenda kusizitiza kuwa Biblia ni kitabu yatima kisichokuwa na Mtume au Nabii, sasa lazima kila atakaye kuwa wakili wa Biblia awe na Kanisa lake au Imani tofauti na wale wengine, mfano wengine ni jumamosi, na wengine jumapili. Wengine husema Yesu [Alahi salaam] mwana wa maryam ni mungu, na wengine husema mwana wa mungu au ni mungu tena ni mwana wa mungu!.
Sote ni viumbe vya Allah [Subhanahu Wata'ala], naye ametuweka katika daraja mbali mbali kwa kadiri ya uchaji Mola wako na ushahidi ni Qur'ani 49:13, ‘ .[Mmbora wenu ni Yule anaye mcha Mola’.] Katika hawa wanadamu Allah [Subhana wata'ala] aliwachagua Manabii watakao pewa ujumbe wake ili wawapelekee watu waliotimilizwa kwao, na hao Manabii anao wataja Amos, Ezekiel, Daniel,Samuel, Daudi, Yeremia, Isaiah, Yesu [Alahi salaam] mwana wa maryam, n.k, wote walitumwa kwa wana wa Israeli tu, na hata kama waliandika kama anavyodai basi ujumbe wao bado ni kwa wana wa Israeli tu.
Kudai kuwa Nabii Musa [Alahi salaam] aliandika vitabu vitano vya kwanza katika Biblia , mwanzo, kutoka, walawi, hesabu na kumbukumbu la torati, si kweli kwa sababu katika kumbukumbu Musa [Alahi salaam] anakufa lakini bado anasimulia maziko yake, jambo ambalo haliwezekani kamwe. Ndugu Fondo amka, toka usingizini, kumekucha watu wanasoma, watu wanasilimu hata ndugu zako!. Suhufi kwa kiarabu ni nyaraka, na kwa fondo na wasabato yafaa mjue kuwa Nabii Musa [Alahi salaam] anao utumishi mara mbili, kwanza kwa Firaun aliyejiita mungu Qur'ani [53:36, ] na pili ni Tourati kwa Wana wa Israel, Qur'ani [5:45,] [11:110 ], na sina shaka Fondo nimjuae si katika wana wa Israel!.
Waislam hatusemi, kwa nini Qur'ani iliandikwa, bali twasema , ipi hekima ya Allah [Subhanahu wata'ala] kuifunua Qur'ani, hii ni kwa sababu Mtume [Rehma na amani ziwe juu yake ] alikuwa hajui kusoma wala kuandika, [Quraan 7:157] ‘ [Ambao kwamba wanamfuata huyo Mtume, Nabii, asiye soma wala kuandika, wanaye mkuta kaandikwa kwao katika Taurati na Injili, anaye waamrisha mema na anawakanya maovu, na anawahalalishia vizuri, na ana waharimishia viovu, na anawaondolea mizigo yao na minyororo iliyo kuwa juu yao.]. Wakristu walipoweka fikra hii ya “ kuiandika Biblia ”, haikukoma bali wanaendelea kuikarabati hata leo, nayeye Fondo ajua kwa uzuri kuwa takriban kila kanisa lina Biblia yake tena kwa faida yake tu, na ajabu ni licha ya wao wenyewe kuandika Biblia yao bado hawaiamini kamwe na ni sababu ya Nabii Yesu [Alayhi salaam] mwana wa maryam alipowaambia ‘ kusikia mtasikia wala hamtaelewa ‘, kwa sababu mioyo imesusuwaa, kila mmoja kwa faida yake.
Luka mmoja katika waandishi wa Bibli asema katika utangulizi wake ambao baadhi ya wasomi wa kikristu wanapenda sana kuyahariri asema katika utunzi wake kwa Mfalme Theofilo, “ kwa kuwa watu wengi wametia mikono kutunga kwa taratibu habari ya mambo yale yaliyo timizwa katikati yetu kama walivyo tuhadithia wale waliokuwa mashahidi wenye kuyaona, na watumishi wa lile neon tokea hapo mwanzo, nimeona vema name kwa kuwa nimejitafutia usahihi wa mambo hayo yote tangu mwanzo kukuandikia kwa taratibu, Theofilo mtukufu “. Haya maneno ya kutunga yaweza kuwa ya Mola?, na vipi utayalinganisha na Qur'ani Tukufu ambayo ndio ufunuo wa mwisho kwa wanadamu wote, Qur'ani ndicho kitabu pekee kilicho bakia katika asili yake, na leo twaisoma kama alivyo isoma Mtume Muhammad [Rehma na amani ziwe juu yake ] kinyume na Biblia yenye ‘Versions’ mbali mbali, Qur'ani pekee ndio iliyosimamisha ujumbe wa Tawheed, yaani kumtukuza Mwenyezi Mungu Mmoja tena wa pekee, kinyume na Biblia inayotangaza miungu mitatu [utatu mtakatifu], ni Qur'ani pekee inayo wahimiza Waislam kuwaheshimu na kuwahami Manabii wote, kinyume na biblia inayo wabagua ,kuwasuta na kuwatukana Manabii watukufu na twasema bila uwoga kuwa Qur'ani ni muujiza wa kuendelea tunaoishi nao, na Allah [Subhana wata'ala] Mwenyewe ameapa kuilinda kutokana vitimbi vya akina Fondo na wenzake.
Allah [Subhana wata'ala] ndiye aliyekamilika kwa sifa zote zilizo kamili, kinyume na huyu Mungu ambaye Fondo anamtembeza kwenye kikapu, aliyezaliwa, ana mama mzazi, alikula samaki wa kupaka, alilipa kodi, alilala usingizi, alipigwa makofi, aliuwawa, kasha akadai kufufuka. Allah [Subhana wata'ala] ana uhai wa maisha, ni mjuzi yote yaliyo mbinguni na ardhini, kusinzia hakumshiki wala kulala, hali, ndiye mtoaji Riziki na kwa ufupi amekamilika kwa sifa zote zilizotakasika.
Pope John Paul II, aliandika kitabu “ crossing The Threshold “ mwaka 2000, na ndani yake akawa analalamika na kuona ghere kuwa kila sifa njema zote amepewa Mola wa Waislam!.
Waandishi wa Biblia walilenga kukutoa katika njia sahihi ya Allah [Subhana wata'ala], na kukutumbukiza kanisani, na haya yanadhibitishwa na Paulo anaye shuhudia kuwa alifanya mambo mengi yaliyo pingamana na jina lake Yesu [Alahi Salaam] mnazarethi, ‘ kweli mimi mwenyewe naliona ndani ya nafsi yangu kwamba yanipasa kutenda mambo mengi yaliyopingamana na jina lake Yesu……..’, naam Paulo aliwaita wafuasi wake waende kanisani kinyume na Nabii Yesu [Alahi Salaam] mwana wa maryam aliyehubiri katika masinagogi [misikiti ya wayahoodi], matendo 26:9, luka 4:44, na ushahidi ni katika I wakorintho 4:14-17, ‘ basi nawasihi mnifuate mimi. Kwa sababu hii nimemtuma Timotheo kwenu, aliye mwanangu mpendwa………. Atakaye wafundisha njia zangu…….. kama vile nifundishavyo kila mahali katika kila kanisa.’
Kwa nini Fondo husemi ukweli huu kwa wakristu ili waujue ukweli, kwa nini unaificha kweli hali unaijua?, mtu wa Mungu aweza kukamilika anapo someshwa na kuambiwa uwongo?, kwa nini wabadilisha maandiko kwa manufaa ya kibinasfi?, kesho mbele za Mola Mwenyezi utasema nini?. Nabii Issa Yesu [Alayhi Salaam] mwana wa maryam alipewa kitabu cha Injeel [ kimoja sio vinne], na sisi hatuna shaka kwa hilo, kwako kutumia janja kwa kunukuu mathayo 5:17-18, kasha ukafikiri wajenga hoja ya biblia ni maneno ya kusikitisha. Tourat, Zaburi na Injeel, viliharibiwa na waandishi kama wewe Fondo. Yesu [Alayhi Salaam] mwana wa maryam alimwabudu Mola mmoja kama ilivyosema Tourat, na akawa mwenye kumsujudia Mola, Mathayo 4:10, Marko 12:28-30. Kwanini wawafundisha wakristu na wasabato kumuabudu Yesu [Alayhi Salaam] mwana wa maryam, na kupiga magoti badala ya kusujudu?, je hujaliona andiko hili katika Ufunuo 22:9 “ na wale washikao maneno ya kitabu hiki MSUJUDIE MUNGU”.
Fondo wachekesha, kusema Biblia itadumu mpaka lini. Leo kuna Biblia za Anglican zina vitabu 66,za Roman Catholic zina vitabu 73,za Orthodox zina vitabu kati ya 76 na 84, sasa ipi katika hizi Biblia itadumu milele?, naona kiu kikubwa kwa wakristu na wasabato tafadhali waambie ukweli, lau sivyo utaulizwa na Mola na sijui utamwambia nini.
Kama Waislamu, kila tunapopata nafasi ya kueleza ukweli, kamwe hatutumii Biblia kwa sababu si kitabu cha Mola, japo kuwa kuna baadhi ya maneno yaliyo salimika wakati huo na sijui kama safari hii yatasalimika. Qur'ani 5:44, Allah [Subhanahu wata'ala] alimfunulia Nabii Musa [Alayhi Salaam] kitabu cha Tourat ili kiwe mwongozo kwa wana wa Israel, na walitakiwa wakihifadhi kitabu hicho ili kiwahukumu kwa kila jambo, lakini kikaharibiwa [Qur'ani 11:110] na hao wafuasi wake kwa uzushi wao. Uzushi ni jambo nzito mno na laweza kuwapoteza wengi na mifano tunayo. Bwana Fondo anapo sema na kutangaza kuwa Yesu [Alayhi Salaam] ndiye anayestahili kuabudiwa, ni uzushi mkubwa. Kuharibiwa kwa Tourat hakukutoa nafasi ya kutunga kitabu kingine “ Kumbukumbu la Tourat “ ambacho ni tofauti kabisa na “ Tourat “ aliyopewa Nabii Musa [Alayhi Salaam]. Sio hoja kama Biblia inakubali au haikubali, ukweli ni kwamba waandishi wa Biblia wanaafiki ukweli wa Qur'ani kuwa Tourat aliyopewa Nabii Musa [Alayhi Salaam] “ imekuwa REPLACED” na kumbukumbu la tourat.
NIV study Bible, katika kuto sherehe juu ya Zaburi, wanasema kuwa huenda kuna ukweli kidogo kuwa Nabii Daudi [Alayhi Salaam] aliandika sehemu ya Zaburi hadi sura ya sabini na nane [78], lakini kuanzia sura ys sabini na tisa [79] mwandishi wake hajulikani, na ndio sababu Muislam halazimishwi kuyaamini maandiko ya Biblia, maandiko ambayo ya mtukana Nabii Daudi [Alayhi Salaam] kuwa alikuwa mzinifi [subhana llah], na wengine wenye tama ya utajiri wakajifanya watunzi wa nyimbo za Injeel, kama Daudi alivyokuwa akiimba.
Fondo asema kihakika kuwa Yesu [Alayhi Salaam] mwana wa maryam alipewa Injeel, na SI mathayo, marko, luka wala yohana, [Qur'ani 5:46,] [Qur'ani 57:27,] lakini wakaivuruga matokeo yake leo ni kutoaminiana na kuchanganyikiwa kwa wakristu na kama Paulo alivyo wapata wakristo kwa hila, IIwakorintho 12:16, na Fondo naye anaazimia hilo! Hatuwezi kulinganisha hata kidogo mfumo wa Qur’ani na ule uliofidiwa kwenye Biblia. Yashangaza kuwa na makosa yote pamoja na udhaifu bado Fondo aweza andika mwisho mada hii kuwa japo biblia imeonyesha kuwa mungu atafanya ukahaba, Isaya 23:17, na kuwa Mola alimdanganya Nabii Yeremiah 4:10 na mengi eti bado biblia ina mwongozo sahihi kwa wanaadam!.
IMETAYARISHWA NA :
ADAM AMBETSA
MWEMBE TAYARI TABLIGH GROUP
MOBILE NO. 0723 17 41 54
MOMBASA, KENYA.
MIUJIZA YA YESU
Miujiza imetajwa tukio linalo enda kinyume na taratibu tuzijuazo kama wanadamu, na ni Dalili kutoka kwa Allah[swt] ili waja wajue na kumtambua alowaumba, pia kupitia miujiza Allah[swt] huwatia nguvu Mitume na Manabii wake ili kuwabainisha hao Mitume na Manabii kuwa ni wakweli [Yohana 11:38-44] kinyume na leo ambapo kila mmoja katika jumuiya ya wakristu anauza ‘miujiza ‘ kwenye radio, runinga,magazeti na hata kwenye mitandao.
Mitume wengi na Manabii waliotimilizwa, Allah[swt] aliwajaalia miujiza mbali mbali, na Yesu mwana wa Mariam ni mmoja wao na kabla yake walikuweko Manabii wengi tu na Miujiza mikubwa wala hawakuitwa waungu au wana wa mungu ila walifahamika kwa vyeo vyao tu …Manabii!.
Wana wa Israeli waliletewa Manabii wengi tu, lakini wakawafanyia vitimbi vikubwa kwa kuwaaua baadhi yao, kuwatesa na wengine kuwatoa mijini kwao, na Yesu mwana wa Mariam si wa kwanza, na ukisoma Kumbu Kumbu la Torati 31:27-30, yaonyesha malalamishi ya Nabii Musa Ibn Imran kuwa pindi atakapoondoka wana wa Israeli watageukia ibaada ya masanamu, na kuwaua waliotumwa kwao na Yoshua mwana wa Nun naye aliwaapiza wana wa Israeli wote na shahidi wake ni JIWE lisilokuwa na uhai machoni pao na wakamuona kama mtu aliyetokwa na akili, Yoshua 24:24-28.
Yesu mwana wa Mariam aliwasuta wana wa Israeli kuwa wamefanana na makaburi yaliyo pambwa kwa nje, lakini kwa ndani ni uozo na mifupa ya watu waliomuasi Allah [swt] na Manabii wake, Mathayo 23:27,na Mathayo 23:34-37. Kumhusu Yesu mwana wa Mariam, ushahidi ulioko ni wazi kuwa ni Mtume kwa wana wa Israeli tu, wala si kwako ndugu mkristu,Mathayo 15:21-26, Mtahayo 10:23, Matendo 5:31, na Quraan iliyo teremshwa na Allah[swt] kwa Mtume[saw] takriban miaka mia sita [600] yasadikisha hayo sasa huo ujanja wa kikristu mtaupata wapi?. Allah [swt] anapolitaka jambo lake huliambia "kua na hua" Quraan 36:82, Zaburi 33:6,9,na Quraan 19:35, na Yesu mwana wa Mariam alijaaliwa muujiza wa kutengeza kwa udongo mfano wa ndege akampuliza mara akaruka kwa idhini ya Allah [swt] na ukawa ni muujiza kwa wana wa Israeli kama vile Mama yake alivyofanywa muujiza kwa kumzaa mwanawe Yesu bila kuingiliwa na mume yeyote ila kwa mapenzi yake Allah[swt].
Tafsir ya Ibn Abbass na Qurtubi katika aya hii Quraan 3:48-49, zasema kuwa huo mfano wa ndege alikuwa ni ‘ khufash ‘ popo ambaye japo huruka kama ndege ,hatagi mayai bali hunyonyesha. Twatoa mfano huu kwa sababu wakristu wengi kama wayahoodi hawakumwamini Yesu mwana wa Mariam kama Nabii,kwa hivyo wakampa masharti afanye ndio wapate kuamini, kwetu Waislamu ni kuwa tumesikia na tumetii. Katika maelezo sahihi ya Uislamu ni kuwa Yesu mwana wa Mariam aliwafufua watu watatu pekee, nao ni: Aadhir, Ibn ajuzi [mtoto wa ajuza mcha Mungu na Sam Ibn Nuhu aliyekuwa amekufa karne kadhaa. Wakwanza wawili baada ya kufufuliwa waliishi miaka mingi hata wakawa na familia zao, ama Ibn Nuhu kama angeweza kufufua kimiujiza mtu aliyekufa karne nyingi zilizopita, na kwa uwezo wa Allah [swt] yote yakawezekana na ningependa kusizitiza kuwa kabla ya miujiza yote hii Yesu mwana wa Mariam alikuwa akiswali rakaa mbili kwa Muumba.
Japo Waislam wanazo habari zote hizi kamwe hatuja tokwa na akili na kudai Yesu mwana wa Mariam ni Mungu, na hata kitabu cha wakristu, biblia,chakubali kuwa Yesu mwana wa Mariam si Mungu bali ni Mtumishi tu; Yohana 5:30, Matendo 2:22, Yohana 14:28, Luka 11:20. Bibilia kwa upande wake imeonyesha muujiza wa kwanza wa Yesu mwana wa Mariam alitengeza ‘ Divai ‘ watu wakanywa na kulewa [ Yohana 2:1-11. Kwa maelezo sahih, wako Manabii wengi walio fanya miujiza ya ajabu lakini wao si waola, soma miujiza ya Nabii Musa Ibn Imran, Nabii Yona, Nabii Ezekieli n.k.
Zama za Nabii Yesu mwana wa Mariam kulikuwa na ujuzi mkubwa wa tiba, na matabibu walikuwa wakishindana katika tiba, lakini mambo matatu yaliwashinda nayo ni kufufua waliokufa, mbalanga na upofu wa tangu kuzaliwa. Zama za Mtume[saw] ni zama za ufahamu, balagha na elimu ya hali ya juu na Mtume [saw] akapewa Muujiza mkubwa kuliko yote nayo ni QURAAN, imebakia katika asili ile ile namna ilivyoteremshwa [Quraan 15:9] kinyume na bibilia ambayo ina chapa zaidi ya mia [100]!
IMETAYARISHWA NA :
ADAM AMBETSA
MWEMBE TAYARI TABLIGH GROUP
MOBILE NO. 0723 17 41 54
MOMBASA, KENYA.
Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.