Menu

Itikadi za wakiristo

 

 

JE KUNA DHAMBI ASILI?

 

 

Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na ardhi, aliyewafanya malaika kuwa wajumbe wenye mbawa mbili mbili na tatu tatu na nne nne. Huzidisha katika kuumba apendavyo. Hakika Mwenyezi Mungu ni muweza juu ya kila kitu.

Mijadala ni njia ya kuelewana, kupeana fikra na lazima mijadala ifanywe katika mazingira ya upendo na hamu ya kutaka kujua ukweli, lakini mara nyingi ni vigumu mno kwa kuwa ndugu wakristo huona kutishiwa na nafasi yao kuondolewa au kupoteza wafuasi kwa hivyo hufanya fujo lakini kupitia kurasa hizi ni matumaini yangu kuwa watafaidi.

Lengo la elimu ya ulinganishi (comparative study), na mijadala yetu ni kufichua ukweli, na kuwazindua wale wenye ufahamu haba ili wapate changa moto kwa kuwa sote tuna ufahamu unao pishana kwa hivyo kuwa na misingi na ufahamu ambao hawawezi kuiruka wala kuipinga kwa hali zozote na matokeo yake ni kubuni fikra za ajabu na moja katika hizo fikra za ajabu ni hii tunayo ijadili “dhambi asili”.

Kila anayezaliwa, Allah (s.w.t) anamjaalia ‘Fitrah’ yaani asili ambayo haifisidiwi, na ni wazazi wake ambao humfanya awe yahoodi, mkristo au majusi na kuuacha uislam njia ya haki. Sisi tutajitahidi kama ni kunukuu tuwe waaminifu kwa maandiko ya Quran tukufu au Biblia na kama kuna madai tuthibitishe.

Ndugu wakristo wana madai yasiyo sahihi kuwa watu wanapozaliwa wanarithi kosa la Nabii Adam, hivi kuwa hata kitoto kilichozaliwa dakika hii unaposoma makala haya eti ana madhambi! Je, kuna hakimu yeyote anayeweza kuhukumu mtu ama watu kwa makosa yaliyotendwa na watu wengine maelfu ya karne zilizopita! Ikiwa haiwezekani Je Allah (s.w.t) aweza kuwahukumu watu kwa makosa ya watu wengine?

Mola aliteremsha vitabu kadhaa ili kutoa miongozo kamili pamoja na kutusimulia baadhi ya viswa navyo ni Taurat, Zaburi, Injeel na Quran tukufu lakini kisa cha Nabii Adam (a.s) namna alivyoumbwa na kisa kamili cha kula lile tunda. Quran tukufu:-

“Na kumbuka pale Mola wako mlezi alipowaambia malaika mimi nitaweka katika ardhi Khalifa. Wakasema, utaweka humo atakaye fanya uharibifu humo na kumwaga damu, hali sisi tunakutakaza kwa sifa zako na tunakutaja kwa utakatifu wako? Akasema, hakika mimi nayajua msiyoyajua.”

 (TMQ 2:30)

Quran inaonyesha uhakika wa matukio sahihi pale malaika waliposhindwa majina ya kila unachokiona, Nabii Adam aliyataja na Allah (s.w.t) akawaamuru malaika wamsujudie Adam (a.s) yaani wamwadhimishe kwa ile elimu aliyokuwa nayo:-

“Na wakumbushe watu habari hii tulipowaambia Malaika msujudieni Adam, wakamsujudia wote isipokuwa Iblis, alikataa na akajivuna na tokea hapo alikuwa katika makafiri.”

(TMQ 2:34)

Tukio hili limenukuliwa katika Biblia lakini ajabu ni kuwa si katika vitabu vya mwanzo bali katika Waebrania ni hoja katika nyaraka za Paulo:

“Hata tena amletapo mzaliwa wa kwanza ulimwenguni asema na wamsujudu Malaika wote wa Mungu.” (Waebrania 1:6)

Quran tukufu inatueleza kuwa baada ya Nabii Adam (a.s) na Mama Hawa kuumbwa waliwekwa katika bustani, yaani peponi.

“Na tulisema (baada ya hapa kumwambia Adam) Ewe Adam, kaa wewe na mkeo katika bustani hii (Peponi) na kuleni humo maridhawa popote mpendapo, lakini msiukaribie………………… lakini shetani Yule Iblis aliwatelezesha wote wawili (wakala katika huo mti waliokatazwa” (TMQ 2:25 – 36)

Kwa aya hizi twafahamu wazi kuwa wote wawili walikula katika huo mti, kinyume na waandishi wa Biblia waliosema kuwa aliyekula tunda kwanza ni Mama Hawa, na Nabii Adam (a.s) alimlaumu sana Mama Hawa akimwambia Mola “Yule mwanamke uliyenipa ndiye aliyenipa tunda nikala” naye Mama Hawa alilaumu nyoka kwa kumtelezesha lakini msimamo wetu waislamu ni kuwa wote (Adam na Hawa) wawili waliteleza na kula katika mti huo waliokatazwa, lakini Allah (s.w.t) aliwafunulia namna ya kutaka msamaha:

“Kisha Adam akapokea maneno (ya maombi) kwa Mola wake akaomba na Mola wake akapokea toba yake. Hakika yeye ndiye wa kupokea toba (kwa wenye kutubia)…” (TMQ 2:37)

Ayah hii (TMQ 2:37) inapatikana katika Quran tukufu pekee, na ndio sababu kama waislam hatuamini kwa watu kurithi dhambi kwa kuwa yule mkosa aliomba msamaha na Mola akamsamehe lakini hawakuendelea kuishi peponi. Allah(s.w.t) asema:

“Akasema (Mwenyezi Mungu) shukeni (katika ardhi) nyinyi kwa nyinyi ni maadui, na makao yenu yatakuwa katika ardhi na starehe (pia) mpaka (niutakao mimi Mwenyezi Mungu). Mtaishi humo na mtafia humo na mtatolewa humo (Mtatolewa kuenda akhera kulipwa).

 (TMQ 7:24 – 25)

Hatuwezi kusema kuwa kifo ni matokeo ya kula katika ule mti waliokatazwa kwa kuwa kifo kiliumbwa kabla ya uhai na Allah (s.w.t) na ndio njia pekee ya kuingia ulimwengu wa pili na ni ukweli na hata wewe ndugu mkristo wajua huwezi kufanya dhambi hata kabla hujazaliwa lakini bado twaambiwa kuna dhambi asili!

Torati ya Nabii Musa (a.s) ilikuwa na habari kamili kuhusu ‘dhambi asili’ na sijaelewa kwa nini ndugu wakristo hupuuza ukweli huu kuwa kila mmoja ahukumiwe kwa makosa yake tu:

“Mababa wasiuwawe kwa ajili ya watoto wao, wala watoto wasiuwawe kwa ajili ya baba zao, kila mtu na auwawe kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe.” (Torati 24:16)

Andiko hili linatiliwa mkazo na andiko hili linalosema:

“Ikawa mara ufalme ulipokuwa imara, mkononi mwake aliwaua watumishi wale waliomuuwa mfalme baba yake, ila hakuwauwa watoto wa hao wauaji, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Torati ya Musa, kama alivyoamuru bwana akisema, ‘mababa wasife kwa makosa ya wauwa, wala wana wasife kwa makosa ya mababa, lakini kila mtu atakufa kwa kosa lake mwenyewe.” (2 Wafalme 14:5-6)

Miaka mingi baadaye wakati wa Nabii Ezekiel maneno haya yanapatikana katika Biblia ya wakristo:

“Neno la bwana likanijia tena kusema, Je, maana yake ni nini hata mkatumia mithali hii katika Israeli mkisema, Baba wamekula zabibu mbichi, nao watoto wakatiwa ganzi la meno? Kama mimi niishivyo, asema Bwana Mungu, hamtakuwa na sababu ya kuitumia tena mithali hii katika Israeli. Tazama roho zote ni mali yangu, kama vile roho ya baba ni mali yangu, ndivyo ilivyo roho ya mwana ni mali yangu. Roho itendayo dhambi ndiyo itakayokufa.”

 (Ezekiel 18:1 – 4)

Nabii Ezekiel aendelea kusema, na nina warai wote wasome na kuyaelewa haya maandiko na kuikataa hii fikra isiyokuwa sahihi kuwa kuna dhambi asili.

“Roho itendayo dhambi ndiyo itakayokufa,

Mwana hatauchukua uovu wa baba yake,

Wala baba hatauchukua uovu wa mwanawe, haki yake mwenyewe haki itakuwa juu yake na uovu wake mwenyewe utakawa juu yake.” (Ezekiel 18:20)

Na katika andiko la mwisho katika Ezekiel kuhusu hoja la mwisho katika Ezekiel kuhusu hoja hii ni hili:

“Basi nitawahukumu nyinyi nyumba ya Israeli, kila mmoja kwa kadiri ya njia zake, asema Bwana Mungu.” (Ezekiel 18:30)

Ndugu msomaji ushahidi huu wa kitabu cha Ezekiel kuwa dhambi asili hamna kwa kuwa haiwezekani baba wale zabibu mbichi na meno ya watoto wasiokula  zabibu yatiwe ganzi na yasikitisha kuona watu wengi wasiojali kile kilichoandikwa katika kitabu chao, nami nauliza mbaya ni nani, anayekuongoza ufuate kitabu chako au Yule anayekudanganya kuwa una dhambi asili?

Andiko linguine linalo puuzilia mbali fikra kuwa ipo dhambi asili na kuwa Nabii Yesu a.s. mwana wa Maryam kaja ili kuichukua ni katika Yeremia, nalo lasema:

“Siku zile hawatasema tena baba za watu wamekula zabibu kali na maneno ya watoto yametiwa ganzi, bali kila mtu atakufa kwa sababu ya uovu wake mwenyewe, kila mtu alaye zabibu kali meno yake yatatiwa ganzi.” (Yeremia 31: 29 – 30)

Mimi si mtaalamu wa akili, lakini natoa changa moto kwao watufahamishe kimasomaso kwa nini hawa ndugu wakristo wanaiona haki kisha wanaipuuza na kubuni njia zao wenyewe kisha akawa mkakamavu katika kuutetea uwongo?

Paulo, muasisi wa ukristo na aliyeandika sehemu kubwa ya agano jipya asema wazi kuwa kile kiitwacho ‘dhambi asili’ ambayo kila mkristo anarithi hamna, na wao wakristo wakatunga wimbo katika nyimbo zao kuwa “kila mtu atalichukuwa furushi lake mwenyewe, na kila mtu atatoa habari zake mwenyewe siku ya hukumu.” Paulo asema:

“Bali kwa kadiri ya ya ugumu wako na kwa moyo wako usio na toba, wajiwekea akiba ya hasira kwa siku ile ya hasira na ufunuo wa hukumu ya haki ya Mungu, atakayemlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.” (Warumi 2:5 – 6)

Ikiwa hii ndio hali halisi siku ya hukumu, je yale madhambi asili aliyochukuwa Nabii Yesu mwana wa Maryam ni yapi? Kwa nini wakristo wasimamishwe tena mbele ya Mwenyezi Mungu kisha atoe habari zake, je wakristo wamehadaiwa na mtu Fulani? Paulo asema katika maandiko yake ya II wakorintho 12:16 akisema lakini na iwe hivyo mimi sikuwatemea bali kwa kuwa mwerevu naliwapata kwa HILA. Je hila hii ndio inayoendela hadi leo? Tafakari hayo.

“Kwa kuwa imeandikwa,

Kama niishivyo anena bwana kila goti litapigwa,

Mbele zangu na kila ulimi utamkiri Mungu,

Basi ni hivyo, kila mtu miongoni mwetu atatoa

Habari zake mwenyewe mbele za Mungu.” (Warumi 14:11 – 12)

Katika waraka mwingine wa Paulo kwa wagalatia ambalo ndilo agano jipya Paulo asema:-

“Maana mtu akijiona ni kitu, naye si kitu ajidanganya nafsi yake, lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo atakapokuwa na sababu ya kujisifu ndani ya nafsi yake tu wala si kwa mwenzake. Maana kila mtu atalichukuwa furushi lake mwenyewe……………….

Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi kwa kuwa chochote apendacho mtu ndicho atakachovuna” (Wagalatia 6:3 – 7)

Kwa ushahidi huu, je wale wanapiga vifua wakidai Yesu amewaondolea dhambi alipowaokoa miaka kadhaa iliyopita wanamfanyia Mungu dhihaka! Je wanasema kweli?

Tutaimaliza sehemu hii ya Biblia kwa andiko moja lisemalo:-

“Tukisema kwamba hatuna dhambi,

Twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu.

Tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi,

Twamfanya yeye kuwa muongo wala neon lake halimo mwetu” (Waraka I Yohane 1:8 – 10)

Paulo asema katika nyaraka zake mambo ya kisawa:-

“Jaribuni mambo yote, lishikeni lililo jema.” (Wathesalonike 5:21)

Ni kweli kuwa Mungu si wa mchafuko, bali wa amani huu mchafuko na kuchanganyikiwa kwatoka wapi hadi wakristo wasijue kuwa hakuna dhambi asili? Je kuna mambo yasiyo mema kwenye Biblia?

Uislamu haukutufundisha katu kuwa kuna mtu anayeweza kubeba au kuchukua madhambi ya mtu/watu, bali Mola alituonyesha kuwa japo sisi twaingia katika madhambi la kufanya ni kumrudia na kusema:-

“Sema, Enyi waja wangu mliojidhulumu nafsi zenu! Msikate tama na rehma ya Mwenyezi Mungu bila shaka Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote, hakika yeye ni mwingi wa kusamehe na mwingi wa kurehemu. Na rejeeni kwa Mola wenu na mnyenyekee kwake kabla ya kukujieni adhabu kisha hamtanusuriwa.” (TMQ 39: 53 – 54)

Kwa ndugu wakristo wanadai kuwa Nabii Yesu a.s. ndiye wa kuzoa madhambi yao na hawaoni haya wakidai hayo bali wengine hata wamethubutu kudai wanaweza kusamehe wakosa madhambi yao kwa ‘malipo’ ya elfu kadhaa.

Nabii Adam (a.s) alipogundua kosa lake haraka alimrudia Mola ili kutaka toba na ayah hii iko katika Quran tukufu pekee, akisema:

“Wakasema ‘Mola wetu! Tumedhulumu nafsi zetu na kama hutusamehe na kuturehemu bila shaka tutakuwa miongoni mwa wenye hasara (kubwa kabisa)’. Akasema (Mwenyezi Mungu) shukeni (katika ardhi) nyinyi kwa nyinyi ni maadui na makao yenu yatakuwa katika ardhi na starehe yenu (pia) mpaka muda (niutakao).” (TMQ 7: 23 – 24)

Uislam umefundisha ukweli wote ili kila aliyepiga shahada ajue kuwa kila analolifanya litamrudia ikiwa ni la kheri au shari. Mola asema:-

“Wala hatabeba mbebaji mzigo wa mwingine (kila mtu atachukuwa jukumu la dhambi zake mwenyewe) na kama aliyetopewa na mzigo wake akimwita (mwingine) kwa ajili ya mzigo wake (amchukulie) hautachukuliwa hata kidogo (na mtu huyo) ingawa ni jamaa yake…………………”

(TMQ 35:18)

Na katika aya nyingine Mola aweka wazi kwa wale wasiyoelewa haya makubwa kuwa ni muhali kwa mtu awaye yeyote kuchukuwa dhambi za mwingine na hili twapenda ndugu wakristo wajue:

“Na mwenye kufanya dhambi, basi ameifanyia nafsi yake (uovu) na Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye na ndiye mwenye hekima. Na mwenye kufanya hatia (ndogo) au dhambi (kubwa) kisha akamsingizia (nayo) asiye na kosa, basi kwa yakini amebeba dhulma kubwa zilizodhahiri.” (TMQ 4: 111 – 112)

Kwa andiko hili ni wazi kuwa ndugu wakristo wana hatia kwa kumsingizia Nabii Yesu (a.s) mwana wa Maryam kuwa ndiye kachukuwa madhambi yao, dhulma juu ya dhulma lakini mwenye kutenda wema basi ni kwa ajili ya nafsi yake (mwenyewe) na mwenye kufanya uovu ni juu yake (mwenyewe) kisha mtarudishwa kwa Mola wenu.

Ikiwa mja ataongoka na kuishi maisha anayotaka Mola ni faida yake tu, na kuwa Allah (s.w.t) alikwisha tuletea Manabii waliotoa bishara na kuonya wale wapendao ubwete wakome. Hatuna shaka kuwa wale wasomao kurasa hizi wameshafahamu kuwa hakuna dhambi asili wala hii fikra kuwa ‘Baba wamekula zabibu mbichi na meno ya watoto yakatiwa ganzi’. Namaliza kwa aya hii:

“Anayeongoka basi anaongoka kwa maslahi ya nafsi yake mwenyewe, na anayepotea basi anapotea kwa hasara (ya nafsi) yake mwenyewe, wala hatabeba mbebaji mzigo wa mwingine. Na sisi si wenye kuwaadhibu (viumbe)mpaka tuwapelekee mtume (awafahamishe yaliyo haki, basi wayakatae ndipo wanapoangamizwa.”

 (TMQ 17:15)

 

 

Imetayarishwa na:

Adam Ambetsa,

M.T.T.G Mombasa.

Mob No: 0723 – 174 154.

 

LOGOISLAM

Search Videos

RSS Content

<

 

WhatsApp This Page Now
 

Visitors Counter

6574700
TodayToday2767
Highest 01-07-2025 : 4073
US
Guests 13

Mkurugenzi na naibu wake

SS10

 

VIKAO VYA OFISI

title_6828ff708ccaf18566864131747517296
title_6828ff708cd9d2685109901747517296
title_6828ff708ce7e10217083621747517296

NISHATI ZA OFISI

title_6828ff708e44411776653511747517296
title_6828ff708e5209465894791747517296
title_6828ff708e5f720084573761747517296 Add content here

HUDUMA MPYA

: 4 + 13 =

IslamChoice- Kiswahili

Ni mtandao mpya wa ulinganizi unao funza mafunzo ya dini ya kiislamu kuambatana na Qur'ani na Sunna za Bwana Mtumeﷺ zilizo sahihi‎ kwa ufahamu wa wema walio tutangulia.

UongofuUongofu.com